>Mwanzo >Soma vitabu >SURA YA KWANZA

SURA YA KWANZA

 

MNYAMA NA HISTORIA YAKE

ONYO LA KUTISHA

Onyo la kutisha mno la adhabu linaloweza kupatikana mahali po pote katika Biblia limo katika Ufunuo 14:9,10: "Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa [alama] katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, yeye naye ATAKUNYWA katika mvinyo ya GHADHABU YA MUNGU iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo."

 Maelezo haya yanaogofya mno na hayafanani kabisa na mafungu mengine yanayoielezea tabia ya Mungu ilivyo, hata tunajikunja kwa hofu. Lakini yanaonyesha wazi kipindi kile ambacho rehema ya Mungu itakapoondolewa kwa wale ambao wanaendelea daima kuikataa mamlaka ya mbinguni. Litakuwa ni tendo lisilo na kifani kwa upande wa Mungu katika uhusiano wake na jamii ya kibinadamu. Kwa karibu miaka 6000 hukumu zake za adhabu juu ya watu walio waovu sana zimechanganywa na rehema Yake. Lakini sasa uovu unafikia kiwango ambacho kinafanya iwe lazima kwa Mungu kuingilia kati, na kukidhihirisha kiwango cha usaliti wa mwanadamu dhidi ya Serikali ya Mungu.

 Hapa ndipo tunataka kujua habari zaidi juu ya dhambi ile inayomfanya Mungu kutenda tendo hilo la ajabu [geni] la kuwaadhibu [waovu] kwa moto. Angalia kwamba jambo hili la mwisho linahusu utii wa uongo kwa mamlaka ile ya Mnyama, ambayo mara nyingi inatajwa katika unabii wa Biblia. Hatimaye dunia hii itasimama ikiwa imegawanyika katika makambi mawili: Wale wanaomsujudu Mungu wa kweli, na wale wanaomsujudu Mnyama yule wa Ufunuo 13. Lakini ni jambo gani linaloleta mgawanyo huo mkubwa wa watu wa dunia hii? Baada ya kueleza ajali itakayowapata waabudu hao wa uongo katika Ufunuo 14:9-11, Yohana analo hili la kusema katika fungu lile linalofuata: "HAPA NDIPO PENYE SUBIRA YA WATAKATIFU, HAO WAZISHIKAO AMRI ZA MUNGU, NA IMANI YA YESU." Hapa tunaona tofauti ya kushangaza kati ya wale wanaomfuata yule Mnyama na wale wanaomfuata Mwana-Kondoo.

 Angalia, tafadhali, ya kwamba suala linalohusika linazunguka juu ya kuzishika amri za Mungu. Wale ambao hawana alama ya Mnyama wanasemwa ya kuwa wanazitii amri hizo [za Mungu], na wale waliobaki wanateseka kwa ghadhabu ya Mungu. Jambo hili linakubaliana kabisa na usemi wa Paulo katika Warumi 16:16, "Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki."

 Wajibu wa hali ya juu unahesabika kwa tendo hili la UTII. Mwishowe, sehemu kubwa ya wakazi wa dunia hii wataikubali mamlaka hii ya bandia ya serikali ya Mpinga Kristo, kwa KUZIASI AMRI ZILE KUU KUMI za Mungu. Rafiki zangu, kila mtu mmoja mmoja atakuwa upande mmoja au mwingine. Biblia inaeleza kwa wazi sana ya kwamba UZIMA au MAUTI utategemea UAMUZI WA MWISHO kuhusu Mnyama huyu wa Ufunuo 13.

Ni ajabu kwamba wanathiolojia wa siku hizi wamepuuzia kabisa UJUMBE HUU WA ONYO wa Ufunuo 14, unaohusu ile Alama ya Mnyama. Shauku ya watu wengi imeharibiwa na mvuto wa WACHUNGAJI ambao hawakutaka kuyachukulia maneno haya ya unabii wa Yohana kwa uzito wake. Mara nyingi wanautupilia mbali [unabii huu] kana kwamba ni waraka wenye utata, usiokuwa na maana, ambao ulilihusu tatizo la mahali pale katika kanisa lile la mwanzo. Kwa sababu fulani kitabu hiki kinachoitwa Ufunuo kinahesabika kama vile ni kitabu kilichofungwa [kisichoweza kueleweka], badala ya ukweli wake wa wazi uliofunuliwa [unaoeleweka] kama jina lake linavyomaanisha. Lakini tafadhali zingatia ya kwamba ahadi imetolewa kwa wale wanaoitafuta kweli iliyomo ndani ya kitabu hiki cha ajabu: "Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu." Ufunuo 1:3.

Kabla ya kukichunguza sana kisa hiki kilicho wazi cha Yohana kuhusu pambano lile la mwisho kati ya Kristo na Shetani, hebu na tutumie muda fulani kuwachambua hao wanaopambana katika vita hii. Ni lini na kwa jinsi gani [pambano hili] lilianza, na kwa jinsi gani litafikia mwisho wake?

 

 WASHINDANI WAWILI WENYE NGUVU

 

Japokuwa kilele cha pambano hili kuu kitafikiwa mwishoni kabisa wa historia ya mwanadamu wakati ambapo dunia yote itakuwa imegawanyika katika makambi mawili yanayopingana, pambano hili kati ya Kristo na Shetani limekuwa likiendelea kwa karibu miaka 6000. Lilianza mbinguni kutokana na uasi wa Lusifa dhidi ya utawala wa Mungu wa ulimwengu wote. Kisa cha malaika huyo mzuri aliyetamani cheo cha Mungu Mwenyezi kimefunuliwa katika Maandiko ya manabii kadhaa wa Agano la Kale. Isaya asema hivi kumhusu kiumbe huyo mwenye utukufu: "Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri [Lusifa], mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, NITAFANANA NA YEYE ALIYE JUU." Isaya 14:12-14.

Mbegu za uasi wa malaika huyo kiongozi, uliojaa ubinafsi, zikaenea kwa kasi sana na kuathiri utiifu wa malaika wale wengine. Mara hiyo theluthi moja ya jeshi lile la mbinguni ikawa imejiunga na kutoridhika kwa Lusifa, na pambano lile kuu likawa njiani ----- pambano ambalo lingeendelea kwa ukali sana kwa zaidi ya miaka 6000, na ambalo hatimaye lingetaka uamuzi wa kila kiumbe kilicho hai mbinguni na duniani.

 Matokeo ya mara moja ya kutopatana yakawa vita mbinguni ambayo ilifikia kilele chake kwa kumfukuza kabisa Lusifa toka mbele zake Mungu na mbele ya malaika wake watiifu. Yohana analieleza jambo hilo kwa njia hii, "Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule Joka, yule Joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule Joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote, akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye." Ufunuo 12:7-9.

Malaika yule aliyeanguka hakuweza tena kujulikana kama Lusifa, jina lililomaanisha "nyota ya alfajiri" bali Shetani, likimaanisha "adui." Sasa pambano likawa limehamishwa toka mbinguni na kuja chini duniani. Hapa litaendelea mpaka litakapofikia mwisho wake mbaya sana kwa kuwagawa watu wa dunia hii kuwa upande wa au kinyume na Amri za Mungu. Kama vile pambano hili lilivyoanzishwa kwa uasi dhidi ya mamlaka ya Mungu, ndivyo litakavyokwisha kwa watu kukataa katakata mamlaka Yake yaliyowekwa katika Sheria ya Serikali Yake.

Shetani amekuwapo hapa pamoja na malaika zake waovu tangu wakati ule alipofukuzwa toka kwenye mwanga. Kwa hila yake ya kishetani amefanya majaribio ya njia mbalimbali za kupigana vita dhidi ya Mungu na Mpango wake kwa ulimwengu huu. Kwa kutumia njia mbalimbali za siri zenye kudhuru ameendelea na juhudi zake ili kuipindua mamlaka ya Mungu. Kusudi la kijitabu hiki ni kuonyesha kwa wazi mashambulio yake imara ambayo yamekwisha fanywa, na yanayofanywa na Shetani dhidi ya misingi ya ile Kweli.

Kila kizazi kimeshuhudia onyesho jipya la nguvu ile ya uovu katika vita yake bila kuchoka dhidi ya programu ile ya Mbinguni ya kuuokoa ulimwengu huu. Sura ya mwisho ya upinzani huu wa adui itakuwa ni ile ya Mnyama wa Ufunuo 13. Mamlaka ile ya bandia [uongo] itasimamishwa kupambana vikali sana na Amri za Mungu. Ulimwengu wote utatakiwa KUCHAGUA upande huu au ule. Muungano huo wa [nguvu za] uovu utajiimarisha kwa pambano lile la mwisho linalohusu utii wa wakazi wa ulimwengu huu. Mambo [yote] yatakuwa yamewekwa wazi, na hakuna hata mmoja ambaye hatachagua upande wo wote. UTII KWA MUNGU au KWA SHETANI, kama alivyodhihirishwa katika mamlaka ile ya Mnyama, utakuwa ndiyo nafasi ya pekee kwa mwanadamu ya kuchagua kati ya mambo mawili yaliyo mbele yake.

 

NI SUALA LA KUFA NA KUPONA

 

Sasa, tukiwa tumepata maelezo machache ya kihistoria ya nyuma ya hao wanaopambana, hebu na tuangalie kwa karibu zaidi mpangilio wa Biblia kuhusu pambano hili la mwisho la mkataa [kuamua mshindi ni nani] katika pambano lile kuu [lililoanza mbinguni]. Tafadhali zingatia ya kwamba Mnyama wa Ufunuo 13 anawakilisha mamlaka kubwa sana ya MPINGA KRISTO ambayo inajaribu kumwondoa Mungu kabisa. Hapa pana maelezo ya mamlaka ile katika lugha ya Ufunuo 13:1-7 [Toleo la King James], "Nami nikasimama juu ya mchanga wa bahari, kisha nikaona Mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba [taji] kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. Na yule Mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, YULE JOKA AKAMPA NGUVU ZAKE NA KITI CHAKE CHA ENZI NA UWEZO MWINGI. Nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstaajabia Mnyama yule. Wakamsujudu yule Joka kwa sababu alimpa huyo Mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule Mnyama wakisema, Ni nani afananaye na Mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye? Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru.

Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake MIEZI AROBAINI NA MIWILI. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa KUFANYA VITA NA WATAKATIFU NA KUWASHINDA, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa."

Hapa hatuwezi kushindwa kuuona ukubwa usio na kifani wa upinzani huu dhidi ya Mungu na dhidi ya wale wanaomfuata. Baadaye katika sura hii hii, tutasoma kwamba mamlaka hii ya Mnyama itakuwa na ushawishi mkubwa sana juu ya dunia nzima, kiasi cha kuwafanya wanadamu kupokea alama [chapa] katika vipaji vya nyuso zao au katika mkono wao [wa kuume]. (Ufunuo 13:16). Mwishoni, wale walio na alama hiyo WATATESWA KWA GHADHABU YA MUNGU ISIYOCHANGANYWA NA MAJI kama ilivyoelezwa katika Ufunuo 14:9,10. Ghadhabu ya Mungu imefafanuliwa zaidi katika Ufunuo 15:1 kwa maneno haya, "Malaika saba wenye MAPIGO SABA YA MWISHO; maana katika hayo GHADHABU YA MUNGU imetimia."

Hali ya kutisha ya mapigo hayo na maumivu makali mno watakayopata wale wanaoipokea chapa [alama] ya Mnyama yamewekwa wazi katika sura ile ya kumi na sita ya Ufunuo. Hatutaongea kirefu juu yake kwa wakati huu, ila na tujikumbushe wenyewe ya kwamba jambo hili litahusu uzima wa milele au mauti kwa wote. Ni kwa bidii ilioje, basi, tungetafuta sana kuelewa Mnyama huyo anawakilisha kitu gani, na jinsi tunavyoweza kuikwepa chapa ile. Pasiwe na kubahatisha au kukisia ko kote juu ya somo hili la maana sana. Yatupasa kujua kabisa hatari iko wapi, na jinsi gani tunaweza kuikwepa.

Mkristo wa kawaida hajapata hata kusikia juu ya umuhimu wa somo hili [kwa maisha yake ya milele]. Hana wazo hata kidogo juu ya Mnyama huyo wala chapa yake, japokuwa maisha yake ya milele yanategemea jambo hilo. Makundi na makundi ya wahubiri wanawafariji watu katika UJINGA wao kuhusu suala hili. Wanasema, "Usiwe na wasiwasi wo wote juu ya Mnyama huyo. Ni jambo gumu sana kulielewa. Mradi tu wewe uzidi kumpenda Bwana utakuwa salama. Huwezi kujua kwa kweli Mnyama huyo ni nani." Sikiliza! Je, Mungu anaweza kutuonya sisi juu ya Mnyama huyo wa kutisha ----- na kisha atuambie ya kwamba haiwezekani kujua huyo ni nani? Je, angeweza kutuambia, "Mtatupwa katika ziwa la moto kama mnayo chapa yake, ila sitawaambia huyo ni nani, ----- ni bahati mbaya sana kwenu kama mnayo [chapa yake]"? La, huyo si Mungu. Yeye anatuonya juu ya hatari ambayo inaweza kuepukwa. Tunaweza tu kujua kwamba sisi tuko salama mbali na Mnyama huyo kama tunamjua Mnyama huyo ni nani. Tunaweza tu kujua kama sisi tumeondokana na chapa [alama] yake kama tunajua chapa yake ni kitu gani.

 

NI MNYAMA WA MFANO TU

 

Je, yawezekana kujua Chapa [Alama] ya Mnyama huyo ni kitu gani? Twaweza kujua, pasipo kukosea, na ni lazima tujue. Lakini, yatupasa kwanza kuelewa kitambulisho cha Mnyama huyo wa unabii. Hebu na tuweke msingi kwamba Mnyama huyo wa ajabu mwenye tabia kadhaa asichukuliwe kama ni mnyama halisi. Hakuna aliyemwona mnyama aliye na mwili wa chui, kinywa cha simba, na miguu ya dubu. Vitabu vya unabii vya Biblia vinatumia MIFANO na ALAMA (ISHARA). Mnyama huyo anawakilisha kitu fulani. Lakini, je! yeye anawakilisha ishara ya kitu gani hasa? Hapa hatutakiwi kubahatisha. Biblia haiachi mwanya wo wote wa kuwa na mashaka [juu ya jambo hili]. Biblia inajifafanua yenyewe kama komentari ya Mbinguni, nayo inatupatia ufunguo wa kuuelewa unabii wote.

Katika maelezo ya Biblia kuhusu Mnyama huyo kila kitu chake kimewekwa katika mifano. Kwa mfano, fikiria yale maji anamotoka Mnyama huyo. Yanawakilisha nini? Soma jibu katika Ufunuo 17:15, "Kisha akaniambia, Yale MAJI uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni JAMAA na MAKUTANO na MATAIFA na LUGHA." Hakuna uwezekano wa kulikwepa suala hili la msingi juu ya jambo hili. Mungu alieleza kwa wazi maana ya maji katika [lugha ya] unabii. Mara tu mfano mmoja unapotafsiriwa katika unabii uwao wote ule, basi, KANUNI hiyo hutumika katika kila unabii mwingineo. Maji daima yatakuwa mfano wa watu katika lugha hii ya mafumbo ya unabii wa Biblia.

Sasa, namna gani juu ya sehemu nyingine za Mnyama huyo wa ajabu wa kitabu cha Ufunuo? Je, zinawakilisha kitu gani? Ili kumjua Mnyama huyo, yatupasa kurudi nyuma kwenye kitabu kile cha Agano la Kale cha Danieli na kulinganisha Maandiko kwa Maandiko [mengine]. Vitabu vya Danieli na Ufunuo kila kimoja kinakifafanua kingine. Vinapatana kabisa kama mkono na glavu [mpira wa kuvaa mkononi] yake. Zingatia, tafadhali, ya kwamba Danieli alikuwa na maono yanayofanana na yale ya Yohana. Hayo yameelezwa katika Danieli 7:2,3: "Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa. Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa aina mbalimbali." Aliyaona maji yale ya unabii kama vile Yohana alivyoyaona, ila Danieli aliwaona wanyama wanne wakitoka baharini [maji mengi] badala ya mmoja tu.

Tumekwisha kuona tayari ya kwamba maji ni mfano wa watu [jamaa] au makutano, lakini, je! wanyama hao wanawakilisha nini? Jibu linapatikana katika fungu la 17, "WANYAMA hao wakubwa walio wanne ni WAFALME wanne watakaotokea duniani." Angalia! Maelezo ni ya wazi kabisa hata hakuna ye yote anayeweza kuuliza swali au kuona mashaka! Mungu anasema kwamba WANYAMA katika unabii wanayawakilisha MATAIFA. Kama vile sisi tulivyo na TAI wa Kimarekani (American Eagle), na Warusi walivyo na DUBU katika msamiati wa kisasa wa masuala ya KISIASA [Tanzania tunaye TWIGA], Mungu naye aliwatumia wanyama zamani, zamani sana kuziwakilisha nchi. Basi, ili kuwa wazi zaidi, Mungu aliongeza maneno haya katika fungu la 23; "Huyo mnyama wa nne atakuwa ni UFALME wa nne juu ya dunia." Kama mnyama yule wa nne anaiwakilisha dola ile ya nne ya historia, basi, wale watatu wa kwanza wangepaswa kuziwakilisha dola zile za kwanza tatu.

Maelezo haya yanarahisishwa zaidi na kueleweka tunapokumbuka kwamba kumekuwa na dola nne tu zilizotawala dunia yote katika historia yote ya dunia hii. Mara kwa mara falme hizo zinatajwa katika unabii wa Biblia na zinatajwa kwa majina yao hasa katika baadhi ya unabii unaohusika katika kitabu cha Danieli. Angalia Danieli 8:20,21 na Danieli 11:2, kama mifano ya maelezo hayo. Katika sura ya pili ya Danieli falme zile zile nne za dunia zinaonyeshwa kwa mfano wa madini nne katika sanamu ile kubwa aliyoiota [Mfalme] Nebukadreza. Dola hizo nne ni BABELI, UMEDI-UAJEMI, UYUNANI na RUMI.

 

DOLA NNE ZA HISTORIA

 

Je, unaweza kuwaangalia kwa karibu zaidi wanyama hao, mmoja mmoja, kama walivyotokea [baharini] katika maono ya nabii yule? Wa kwanza alikuwa "kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai." Danieli 7:4. Hapa tunaona inawakilishwa Dola ile tukufu ya BABELI, ikifananishwa vizuri na yule mfalme wa wanyama [simba]. Ilikuwa ni mojawapo ya dola tajiri kuliko zote, taifa lenye nguvu kuliko yote lililopata kuwamo duniani humu. Angalia kwamba mnyama huyu ana mabawa. Kwa mujibu wa Yeremia 50:44, "MABAWA" katika unabii yanawakilisha KASI [Habakuki l:6-8]. Na kwa hakika, Babeli iliinuka kwa haraka sana na kuchukua nafasi yake kama mtawala wa ulimwengu wote.

Kuanzia 606 K.K. mpaka 538 K.K. Babeli iliendelea kuwa na mamlaka yake yaliyokuwa yameenea kote. Danieli akamwona mnyama wa pili, "kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake." Danieli 7:5. Kwa haraka sana kufuatia nyayo za Babeli ulikuja ufalme wa Umedi-Uajemi mwaka ule wa 538 K.K., hii ni Dola ya ulimwengu ya pili.

Dubu huyo ameinuliwa upande mmoja kuelezea ukweli kwamba Uajemi ilikuwa na nguvu zaidi kuliko Wamedi. Mamlaka zile mbili ziliungana pamoja kuitawala dunia yote. Zile MBAVU tatu huenda zinaonyesha MAJIMBO yale matatu ya ufalme ule ----- BABELI, LYDIA, na MISRI [ambayo waliyateka kwa ukatili].

Kisha katika mwaka ule wa 33l K.K. Umedi-Uajemi iliangushwa chini, na Dola ya tatu ya ulimwengu ikainuka. Kulingana na unabii huu, "[i]kapewa mamlaka." Fungu la 6. Ilikuwa "kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne." Fungu la 6. Mtoto ye yote wa shule aliyejifunza masomo yake ya HISTORIA YA KALE (Ancient History) kwa makini atajua kwamba UYUNANI [Ugiriki] ilijitokeza kama mtawala wa ulimwengu aliyefuata. Iskanda Mkuu (Alexander the Great) alikuja akitembea kutoka nchi ile ya mashariki [ya kati] akiiweka dunia yote chini ya miguu yake kwa muda mfupi sana.

Mabawa yale manne ya chui yanaonyesha kasi kubwa sana aliyokuwa nayo Iskanda katika kuyashinda mataifa [vitani]. Katika kipindi cha miaka minane alikuwa ameushinda kabisa ulimwengu, na kukaa chini akilia kwa sababu hapakuwa na nchi nyingine zaidi za kuzishinda. Walakini yeye hakuweza kujishinda [kujitawala] mwenyewe; alikufa akiwa kijana wa miaka thelathini na mitatu tu kwa ulevi. Wakati wa kufa kwake ufalme wake uligawanywa miongoni mwa majenerali wake wakuu wanne, Cassander, Lysimachus, Seleucus, na Ptolemy. Vichwa vinne vya mnyama huyu vinawakilisha mgawanyo huo wa dola yake. Hilo linatufikisha kwenye mwaka wa 168 K.K., na kwenye anguko la Dola ile ya Kiyunani katika mwaka ule ule. Mpaka hapo, maelezo ya kila kitu katika unabii huo yametimizwa kabisa.

 

MNYAMA WA KUTISHA WA NNE

 

Hebu sasa na tuangalie kule kutokea kwa mnyama yule wa nne, ambaye ni "ufalme wa nne juu ya dunia." Fungu la 23. Japokuwa Danieli alikuwa amewaona wanyamapori hai kama wale walioonyeshwa katika mifano mitatu ya kwanza ya unabii huu, alikuwa hajapata kuona kitu cho chote kinachofanana na mnyama huyu wa kutisha wa nne. Biblia inamweleza kwa njia hii: "Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mnyama wa nne, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake:... naye alikuwa na pembe kumi." Fungu la 7.

Kama tulivyokwisha kujifunza tayari, huyo anaiwakilisha Dola ile ya nne ya ulimwengu, ambayo ilikuwa ni UFALME WA CHUMA wa Rumi. Kuenea kwa ukatili wa utawala wake ulimwenguni kumeandikwa vizuri, kumbukumbu zake, katika kurasa za historia ya kale. Walakini taifa hili kubwa nalo pia lilikuwa ligawanyike kama fungu la ishirini na nne linavyoonyesha. "Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka WAFALME KUMI." Tafadhali zingatia kwamba hiyo ni tafsiri ya Mungu kuhusu zile pembe kumi zilizokuwa juu ya mnyama huyo. Rumi ilikuwa igawanyike katika sehemu kumi.

Kwa kufuata mkondo wa historia tunagundua ya kwamba kutimizwa kikamilifu [kwa mgawanyo huo] kulitokea katika mwaka ule wa 476 B.K.. Makabila makali sana yalishuka kutoka katika nchi ya kaskazini, na kulishinda eneo [la Rumi] la Ulaya Magharibi, wakiligawa sawasawa katika sehemu zile kumi. Sehemu hizo, kusema kweli, zinahusiana na vidole vile kumi vya sanamu ile kuu ya Danieli 2.

Wanafunzi wote wa historia wanafahamu vizuri sana majina ya makabila yale yaliyoishinda Ulaya Magharibi mwaka 476 B.K.. [Makabila hayo] yalikuwa ni Waanglo-Saksoni (Anglo-Saxons) [Waingereza], Waalemani (Alemanni) [Wajerumani], Waheruli [Heruli], Wavandali (Vandals), Waostrogothi (Ostrogoths), Wavisigothi (Visigoths) [Wahispania], Wasuevi (Suevi)[Wareno], Walombadi (Lombards) [Waitalia], Waswisi (Burgundians) [Switzerland], na Wafaransa [Franks]. Saba kati ya makabila hayo bado yangali yapo mpaka leo hii, yakiwa yamekua na kuwa mataifa ya siku hizi. Bado yanaonekana katika ramani ya Ulaya kama mamlaka zenye nguvu za karne ya ishirini. Matatu kati ya hayo [Waheruli, Wavandali, na Waostrogothi] yalitoweka kabisa katika jukwaa la historia, kama tutakavyojifunza muda mfupi tu ujao.

 

PEMBE NDOGO

 

Sasa tuko tayari kusoma fungu linalofuata la unabii ule, na kutafuta maana ya pembe ndogo katika maono haya ya Danieli. "Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang'olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu." Fungu la 8. Hapa yatupasa kuwa waangalifu sana sana hasa. Yatupasa tusifanye kosa katika kuitambulisha kwa uongo mamlaka hiyo ya pembe ndogo, kwa sababu itajidhihirisha kuwa ni ile mamlaka kuu ya Mpinga Kristo iliyotajwa katika historia.

Ili kuepukana na makosa yote ya kuitambulisha, lingekuwa jambo jema kwetu kufikiria kwanza ishara za tabia yake zipatazo tisa ambazo zimeelezwa katika unabii huu huu. Ishara hizo za kuitambulisha [pembe ndogo] zitatuwezesha kuwa na hakika kabisa na tafsiri yake. Hatudiriki kubahatisha au kukisia kuhusu uthibitisho wa historia wa hiyo "pembe ndogo" ya unabii huu.

KWANZA kabisa, pembe ile ndogo ilizuka [ilitokea] miongoni mwa pembe zile kumi. Jambo hilo linaiweka [pembe ndogo] kijiografia katika eneo la Ulaya Magharibi. PILI, ilizuka "kati yao." Kwa kuwa pembe zile kumi zilitokea mwaka ule wa 476 B.K., pembe ile ndogo ingeanza utawala wake kipindi fulani baada ya mwaka ule. TATU, ingeyang'oa matatu kati ya yale makabila kumi wakati wa kutawala kwake. Fungu lile la nane linasema kwamba mbele yake ile pembe ndogo "pembe tatu katika zile za kwanza zikang'olewa kabisa."

NNE, pembe ndogo ingekuwa na "macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu." Fungu la 8. Hii inaonyesha kwamba mwanadamu angeiongoza mamlaka hiyo iliyowakilishwa na pembe ndogo. TANO, "Naye atakuwa mbali na hao wa kwanza [wafalme kumi wa kwanza]." Fungu la 24. Hii inamaanisha kwamba pembe ndogo ingekuwa ni mamlaka tofauti na zile falme za kisiasa tu ambazo zilikuwa zimeitangulia. Tabia ya SITA inafunuliwa katika sehemu ya kwanza ya fungu lile la ishirini na tano, "Naye atanena maneno KINYUME chake Aliye juu..." Fungu lingine linasema, "maneno makuu, ya makufuru" Ufunuo 13:5.

Kufikia hapa, labda tungeeleza kwa kutumia Biblia maana ya MAKUFURU. Katika Yohana 10:30-33, Yesu alikuwa karibu kupigwa kwa mawe kwa kudai kuwa Yeye alikuwa UMOJA NA BABA. Wayahudi waliokuwa tayari kumwua walisema, "Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa KUKUFURU, na kwa sababu WEWE ULIYE MWANADAMU WAJIFANYA MWENYEWE U MUNGU." Kulingana na fungu hili ni kukufuru kama mwanadamu akipewa mahali pa Mungu.

Hebu sasa na tusome maana nyingine ya kukufuru. Yesu alikuwa amemsamehe mtu mmoja dhambi zake, na waandishi wale wakasema, "Mbona huyu anasema hivi? ANAKUFURU. Ni

nani anaweza kusamehe dhambi isipokuwa mmoja tu, ndiye Mungu?" Marko 2:7. Ni wazi, Yesu hakukufuru, kwa sababu alikuwa Mungu, alikuwa na uwezo wa kusamehe dhambi. Lakini kwa MWANADAMU kutoa madai hayo lingekuwa jambo la KUKUFURU, kwa mujibu wa maelezo ya Biblia yenyewe.

Sasa tunakuja kwa ile ishara ya SABA ya kuitambulisha [pembe ndogo], hiyo tunaipata vile vile katika fungu la ishirini na tano, "Naye atawadhoofisha watakatifu Wake Aliye juu." Hilo linaonyesha kwamba pembe ndogo ni mamlaka INAYOTESA watu. Itafanya vita na watu wa Mungu, na kuwafanya WAUAWE. Ishara ya NANE pia inatolewa katika fungu la ishirini na tano, "Naye ataazimu kubadili majira na sheria." Ni wazi, katika upinzani wake mkali dhidi ya Mungu Aliye Mbinguni, kwa kunena maneno makuu dhidi Yake, mamlaka hii pia inatafuta KUIBADILI SHERIA KUU ya Mungu. Kitendo hiki cha pembe ndogo kingeweza tu kuwa JARIBIO (ATTEMPT) la kufanya badiliko hilo. Ni wazi, Sheria ile ya Maadili ya Mungu HAIWEZI KAMWE KUBADILISHWA NA MWANADAMU.

 

UTAWALA WAKE WA MIAKA 1260

 

Ishara ya TISA, na ya mwisho ya kuitambulisha [pembe hiyo ndogo], katika fungu la ishirini na tano, hutuambia kabisa kwa muda gani pembe hiyo ndogo ingeyatumia mamlaka yake juu ya dunia hii, "Nao watatiwa mikononi mwake kwa WAKATI, NA NYAKATI MBILI, NA NUSU WAKATI." Hapa tumekabiliwa na usemi wa ajabu. Kwa kweli ni usemi ambao Biblia yenyewe inaufafanua. Katika Ufunuo 12:14, tunasoma maneno haya kuhusu kipindi kile kile cha wakati: "Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa WAKATI NA NYAKATI NA NUSU WAKATI, mbali na nyoka huyo." Sasa soma fungu la sita, ambalo linalieleza tukio lilo hilo. Badala ya kusema, "wakati na nyakati na nusu wakati," linasema, "siku elfu na mia mbili na sitini." Kwa hiyo tunaona ya kwamba vipindi hivyo viwili vya wakati VINAFANANA KABISA. Kwa kuyalinganisha Maandiko hayo, tunaelewa kwamba wakati mmoja ni mwaka mmoja. Hilo hutupatia nyakati 3 1/2, au miaka 3 1/2, kwa sababu miaka 3 1/2 ni sawasawa kabisa na siku 1260. Naam, tunatumia mwaka wa Biblia ulio na siku 360.

Sasa tuko tayari kutumia KANUNI nyingine kuu ya kutafsiri unabii huu. Tafadhali zingatia siku zote ya kuwa katika kupima wakati wa unabii, Mungu anatumia siku moja kuwakilisha mwaka mmoja. Katika Ezekieli 4:6 tunaisoma kanuni hiyo, "Siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia." Kuungwa mkono zaidi tunakupata katika Hesabu 14:34. Njia hii ya kuhesabu wakati ni lazima itumike siku zote katika somo la unabii wa Biblia. Kwa hiyo, hii inamaanisha kwamba mamlaka ya pembe ndogo ingetawala kwa MIAKA 1260, badala ya SIKU l260 tu.

 

UTIMILIZO HALISI

 

Sasa mbele yetu tunayo orodha ya tabia maalum tisa, ambazo zimetolewa toka katika sura ya saba ya Danieli, ili kuifafanua pembe ile ndogo. Kuna mamlaka moja tu katika historia yote ambayo inapatana kabisa na maelezo yaliyotolewa hapa. Kwa shida mno ishara yo yote katika hizo inaweza kutumika kwa [mamlaka] nyingine, isipokuwa ni UPAPA peke yake. Kanisa Katoliki peke yake linatimiza mambo yote yanayoitambulisha [pembe hiyo ndogo] ambayo yametajwa katika Danieli 7.

Hebu na tuangalie kwa haraka na kuona kwa wazi jinsi jambo hilo linavyotekelezwa. KWANZA kabisa, UPAPA ulitokea [katika eneo la] Ulaya Magharibi, katikati kabisa ya eneo la Dola ya Rumi ya Kipagani ----- katika RUMI yenyewe. PILI, ulizuka baada ya mwaka 476 B.K. wakati Mfalme Justinian alipomteua Papa kuwa mtawala wa KISIASA na wa KIROHO wa ulimwengu wote. Haya ni mambo ya kweli ya historia ambayo yanaweza kuhakikishwa kutoka katika chimbuko la mamlaka yo yote ile ya kihistoria.

TATU, Upapa ulipotokea ulipingwa na makabila matatu ambayo yalikuwa yametawala baada ya kuangushwa kwa Dola ya Kirumi. Wavandali (Vandals), Waostrogothi (Ostrogoths), na Waheruli (Heruli) walikuwa ni mamlaka zenye imani ya Arius (Arian powers) ambao kwa nguvu zao zote walipinga kuzuka kwa Kanisa Katoliki. Majeshi ya Warumi yakayang'oa kabisa na kuyaangamiza makabila hayo matatu. La mwisho katika hayo matatu liliangamizwa katika mwaka ule ule wa 538 B.K., wakati RUMI [YA KIPAPA] ilipoanza kutawala dunia.

NNE, Katika mfumo wake, Kanisa Katoliki lilikuwa na MTU akiliongoza. TANO, Upapa ulikuwa ni UFALME ULIO TOFAUTI na falme zile nyingine za kisiasa zilizoutangulia. Ulikuwa ni MAMLAKA YA KIDINI NA KISERIKALI ambayo iliitawala dunia yote. Hakuna mamlaka iliyofanana kabisa na hiyo ambayo ilipata kuonekana ulimwenguni kabla ya wakati ule.

Sasa tunaiangalia tabia yake ya SITA ----- ile ya kunena maneno makuu na makufuru dhidi yake Aliye juu. Je, Upapa unatimiza maelezo hayo? Tunahitaji tu kukumbushwa kwamba Kanisa Katoliki limejitwalia lenyewe UWEZO WA KUSAMEHE DHAMBI. Kuhusu maneno yake makuu, hebu ninukuu kutoka katika makala ya F. Lucii Ferraris, iliyo katika kitabu cha PROMPTA BIBLIOTHECA CANONICA JURIDICA MORALIS THEOLOGICA. Kitabu hiki kilichapishwa mjini Roma, na kimeidhinishwa na ensaiklopidia ya Kikatoliki. Sikiliza madai haya: "Papa ni mkuu mno, naye ametukuzwa sana, kiasi kwamba yeye si mtu tu, bali kama ilivyo, yeye ni Mungu na Aliye Badala ya Mungu (Vicar of God). Kama ilivyo, PAPA NI MUNGU DUNIANI. Mfalme mkuu wa wafalme, mwenye uwezo mwingi." Gombo la VI, uk.25-29. Haya ni maneno machache tu ambayo Biblia inasema kuwa ni makufuru. UPAPA unatimiza ishara zote za utambulisho na hivyo kuwa ile PEMBE NDOGO.

Sasa tunakuja kwenye kitambulisho cha SABA, tunaona ya kwamba HISTORIA inaunga mkono unabii huu kuhusu MATESO YA PAPA. Kila mmoja anayejua habari za Kizazi kile cha Kati (Middle Ages) [Zama za Giza] anafahamu fika ukweli kwamba mamilioni ya watu waliteswa [kikatili mno] na kuuawa na Mahakama Maalum za Kikatoliki (Inquisitions). Kutoka katika kitabu kilichoandikwa na Kadinali wa Kikatoliki, ambacho pia kimeidhinishwa na Kanisa [Katoliki], tunasoma hivi: "Kanisa Katoliki... lina hofu kuu ya kumwaga damu. Hata hivyo, linapokabiliwa na UZUSHI [HERESY]... LINALAZIMIKA KUTUMIA NGUVU, kutoa adhabu ya kupigwa viboko mwilini, na KUTESA. Linaunda mahakama kama ile ya Inkwizisheni (Inquisition). Linatumia SHERIA ZA SERIKALI kulisaidia... Lilifanya hivyo hasa katika karne ile ya 16 kuhusiana na WAPROTESTANTI... Katika nchi ya Ufaransa, chini ya [wafalme] Francis I na Henry II, katika nchi ya Uingereza chini ya (Malkia) Mary Tudor, [Kanisa Katoliki] liliwatesa wazushi." Maneno haya yamenukuliwa kutoka katika kitabu cha 'THE CATHOLIC CHURCH, THE RENAISSANCE AND PROTESTANTISM', uk.182-184.

Tunaweza kuongeza semi nyingi kama hiyo kutoka kwa wanahistoria, Wakatoliki na Waprotestanti, zinazoelezea MATESO YA KUTISHA ya mamlaka ya kipapa juu ya Waprotestanti. Kwa njia hiyo tunaweza kuona utimilizo kamili wa maelezo haya ya pembe ndogo. Ishara ya NANE, kama ilivyotolewa katika fungu la ishirini na tano, inahusu jaribio lile la kubadili Sheria ya Mungu [Amri Kumi]. Je, jambo hilo linahusika na Upapa? Tafadhali zingatia haya: Kanisa Katoliki limeondoa Amri ya Pili kutoka katika vitabu vyake vya mafundisho ya dini na Katekisimu zake, kwa sababu inashutumu IBADA YA SANAMU. Kisha Amri ya Kumi imegawanywa [sehemu mbili] ili waendelee kuwa na Amri Kumi. Walakini mbili zinakataza KUTAMANI, na hakuna hata moja inayokataza IBADA YA SANAMU. Kwa njia hii, Upapa UMEAZIMU [UMEFIKIRIA] kubadili Sheria ya Mungu, lakini bila mafanikio. SHERIA YA MUNGU HAIWEZI KUBADILISHWA.

Mwishowe, tunakuja kwenye ishara ile ya TISA ya kitambulisho chake, ambayo inatuambia hasa muda ambao mamlaka hii ya Upapa ingeyatumia mamlaka yake juu ya dunia hii. Tuligundua kwamba ingetawala kwa miaka 1260. Je, jambo hilo linakubaliana na [kumbukumbu za] historia? Kumbuka, ya kwamba tumeona jinsi Upapa ulivyoanza utawala wake, kwa amri ya Justinian, katika mwaka wa 538 B.K.. Tukihesabu kuja upande wetu miaka 1260 kuanzia mwaka huo tunaletwa kwenye mwaka wa 1798. Katika mwaka uo huo Jenerali wa Kifaransa, Berthier, aliongoza majeshi yake kuingia mjini Roma na kumng'oa Papa [Pius wa VI] kutoka kwenye kiti chake cha enzi. Alichukuliwa uhamishoni, na mali zote za Kanisa zikataifishwa [zikanyang'anywa]. Uongozi wa Serikali ya Kifaransa ulitoa amri kwamba pasingekuwa na Askofu mwingine wa Roma kamwe. Kwa kadiri ulimwengu ulivyohusika, na kwa mwonekano wa nje, Kanisa Katoliki lilikuwa limekufa. Baada ya miaka 1260 kamili, kwa kutimiza unabii huu, likapoteza utawala wake juu ya dunia hii. Hivyo pointi hii ya mwisho imetimizwa kwa wazi kabisa katika Upapa, na katika Upapa peke yake.

 

MNYAMA NA PEMBE NDOGO WAFANANA

 

Huenda unashangaa kwamba mambo haya yote yana uhusiano gani na Mnyama yule wa Ufunuo 13. Sasa tuko tayari kumtambulisha Mnyama yule mwenye tabia kadhaa aliyeelezwa katika kitabu cha Ufunuo. Hebu na tusome maelezo ya Mnyama huyo kwa mara moja tena, ambaye ana mwili wa chui, miguu ya dubu, na kinywa cha simba. "Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru." Fungu la 5. Angalia, tafadhali, ya kwamba Mnyama huyu anafanya jambo lile lile sawasawa na pembe ile ndogo ya Danieli. Fungu la tano linaendelea kusema hivi: "Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili." Ni muda gani unawakilishwa na miezi arobaini na miwili: Ni siku au miaka 1260 kamili ----- sawasawa na nyakati 3 1/2 za unabii wa Danieli.

Kumhusu Mnyama huyu, tunasoma zaidi maneno haya, "Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda." Fungu la 7. Pia Mnyama huyu ni mamlaka itesayo watu. Kwa maneno mengine, Mnyama wa Ufunuo 13 ni mamlaka ile ile ya pembe ndogo. Wote wawili huuwakilisha Upapa. Hii ni picha [katuni] ya mamlaka ya Upapa kama ilivyotolewa na Mungu, ikionyesha wakati ule [Upapa] ulipotumia mamlaka yake kwa njia ya kidikteta juu ya dunia yote kwa miaka 1260.

Mlandano [kufanana] wa ziada unapatikana kwa kusoma Ufunuo13:3, "Nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstaajabia Mnyama yule." Kama tulivyokwisha kuthibitisha, jeraha la mauti alipewa mwaka ule wa 1798 B.K., wakati majeshi ya Kifaransa yalipomchukua Papa [Pius wa VI] na kumpeleka uhamishoni [kule Ufaransa]. Lakini jeraha lile lingepona, na mwishowe dunia yote ingetoa UTII wake kwa UPAPA tena. Unabii ule umetimizwa sawasawa kabisa mbele ya macho yetu.

Ulikuwa ni mwaka ule wa 1929 Mussolini alipotekeleza Mapatano (Concordat) yale ya mwaka wa 1929 kati yake na Papa, akimrudishia mali yote iliyokuwa imetwaliwa kutoka mikononi mwa Kanisa. Wakati ule Papa akafanywa kuwa mfalme tena, na Mji Mkuu wa Vatikana (Vatican City) ukaanzishwa kama [makao makuu ya] mamlaka yake ya KISIASA. Tangu siku ile mpaka leo, uwezo wa Upapa umekuwa ukizidi kuongezeka kwa hatua kubwa sana.

Wakati huu wa sasa karibu nchi zote za dunia zinao wawakilishi wao wa kisiasa [mabalozi] katika Mji Mkuu wa Vatikana. Ushawishi usiosadikika wa Upapa katika mambo ya ulimwengu unashuhudiwa katika magazeti ya siku hizi. Karibu kila usemi wa Papa unachapishwa na kusambazwa kwenye miisho ya dunia, na mamilioni kwa mamilioni ya watu wanaitazamia mamlaka hii ya Kipapa kama ni uongozi mkuu mno katika siasa leo. Naam, jeraha limepona hakika, na ulimwengu unaendelea kumfuata Mnyama huyu.

 

Related Information