>Mwanzo >Soma vitabu >SURA YA NNE

SURA YA NNE

IV. MAREKANI (U.S.A.) KATIKA UNABII

 

Mtu ye yote angejivunia kuwa Mmarekani. Kwa kweli hakuna sehemu yo yote duniani ambako watu wake wanaufurahia uhuru kamili kama katika nchi yetu ya Marekani (United States of America). Je, umepata kustaajabu kwa nini jambo hilo ni la kweli? Kuna sababu yake ya kutokea DEMOKRASIA katika sehemu hii ya dunia. Sio bahati nasibu tu kwamba Amerika ni mji mkuu wa uhuru katika ulimwengu mzima. Kwa kweli, Mamlaka ile ya Mnyama ya Ufunuo kumi na tatu ilihusika sana na kutokea kwa [taifa hili la] Amerika.

Unaweza kuwa unajiuliza mwenyewe, "Kwa vipi mamlaka hii ya Papa imehusika na kuwako kwa Marekani?" Ilikuwa ni kwa sababu ya MATESO ya Mamlaka hiyo ya Mnyama kule Ulaya [Magharibi] hata ikatokea Marekani. Mababa Wasafiri (Pilgrim Fathers), ili KUYAKWEPA MATESO ya kidini ya Papa, walikimbilia kwenye Ulimwengu Mpya wa Amerika ambako wangeweza kufuata DHAMIRI zao katika kumwabudu Mungu wao.

Hebu sasa na tupate picha kutoka kwenye kurasa za unabii katika Neno la Mungu. Mafungu kumi ya mwanzo ya Ufunuo kumi na tatu yanaeleza jinsi Upapa ulivyoanza na kutwaa mamlaka yake. Tumekwisha kujifunza tayari unabii huu kwa kinaganaga. Fungu lile la kumi linafunga kwa maelezo ya kukamatwa mateka [mahabusu] kwa Papa [Pius wa VI) katika mwaka ule wa 1798. "Mtu akichukua mateka, atachukuliwa mateka. Mtu akiua kwa upanga, atauawa kwa upanga. Hapa ndipo penye subira na imani ya watakatifu." Kisha mara hiyo Yohana akamwona mnyama yule wa pili katika maono yake, ambaye anamweleza katika fungu linalofuata. "Kisha nikaona mnyama mwingine akipanda juu kutoka katika nchi; naye alikuwa na pembe mbili mfano wa mwana-kondoo, akanena kama Joka." Ufunuo 13:11. Hebu na tuwe waangalifu sana katika kumtambulisha mnyama huyu wa pili. Kuna pointi kadhaa ambazo zitatufunulia utambulisho wa mamlaka hii.

KWANZA kabisa, anaonekana "akipanda juu" wakati ule ule Mnyama yule wa kwanza alipokuwa anapata jeraha lake la mauti. Kwa kuwa Mnyama yule wa kwanza (Upapa) alipata jeraha lake mwaka 1798 wakati Jenerali Berthier alipomkamata mahabusu Papa [Pius wa VI], basi, tungemtafuta mnyama huyu wa pili na kumwona akipanda juu wakati ule. Hii inamaanisha kwamba karibu na mwaka 1798 mamlaka hiyo ingekuwa inajitokeza ulimwenguni. PILI, mnyama huyu wa pili angepanda juu "kutoka katika NCHI." Huyo yuko kinyume na Mnyama yule wa kwanza ambaye alitoka MAJINI. Tuligundua katika Ufunuo 17:15 ya kwamba MAJI yaliwakilisha JAMAA na MATAIFA. Mnyama huyu wa pili, akipanda kutoka katika nchi, angeonyesha picha ya TAIFA likijitokeza katika sehemu fulani ya dunia ambako hakuna ustaarabu [watu] uliotangulia wala halaiki ya watu. Ukosefu wa maji huonyesha uchache wa watu.

TATU, TAIFA hili lilikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, nazo hazikuwa na vilemba [taji] kama zile alizokuwa nazo Mnyama wa kwanza. Alipanda kwa amani, kama mwana-kondoo, na ule ukosefu wa taji [vilemba] huonyesha ya kwamba [taifa hilo] halikuongozwa na wafalme. Halikuwa na utawala wa kifalme, wala utawala wa mabavu [udikteta]. Kila kitu kuhusiana na mnyama huyu kuonyesha utawala wa amani wa KIDEMOKRASIA.

 

MNYAMA WA PILI ATAMBULISHWA

Sasa tuko tayari kumtambulisha mnyama huyu wa pili. Hakuna mashaka yo yote kuhusu utambulisho wake. Kuna taifa moja tu katika historia linalotimiza maelezo hayo. MAREKANI [THE UNITED STATES OF AMERICA] ndilo taifa peke yake lililokuwa "linapanda juu" kupokea mamlaka yake mwaka 1798, wakati Mnyama yule wa kwanza anapata jeraha lake la mauti. Katiba yake ilipitishwa kwa kura mwaka 1787, na Sheria ya Haki za Binadamu ilikubalika katika mwaka wa 1791. Pia, ilikuwa ni katika mwaka ule wa 1798 ambapo taifa la marekani kwa mara ya kwanza lilitambulikana kama ni mamlaka ya dunia. Wanahistoria wanaandika kwamba palikuwa na kitu fulani cha ajabu na cha kudra ya Mungu kuhusu kuinuka kwa nchi hii.

Kwa kutimiza kabisa unabii huu taifa hili lilitokea katika Ulimwengu Mpya, ambako kulikuwa hakuna ustaarabu uliotangulia. Lilikuja kwa amani, kwa njia ya kidemokrasia, na kujikita juu ya kanuni kuu mbili za UPROTESTANTI na SERIKALI YA JAMHURI. Kanisa na Serikali vikawa VIMETENGANISHWA. Babu zetu walikuwa wamechoshwa kuona maovu ya Serikali ile iliyounganisha DINI NA SERIKALI [UPAPA].

Hebu hapa na tusome usemi wa John Wesley, mwanafunzi wa ajabu wa Biblia, na mwasisi wa Kanisa la Methodisti. Akiandika panapo mwaka wa 1754 katika kitabu chake cha "New Testament with Explanatory Notes" baada ya kumfafanua Mnyama wa kwanza wa Ufunuo kumi na tatu kuwa alikuwa anauwakilisha UPAPA, alisema hivi: "Mnyama... mwingine ... Lakini huyo bado hajaja, ingawa hawezi kuwa mbali sana; kwa maana hana budi kutokea mwisho wa miezi arobaini na miwili [1798] ya Mnyama yule wa kwanza." Ukurasa 427. Zingatia, tafadhali, ya kwamba Wesley alikuwa anatazamia kuliona taifa kutokea katika kipindi kifupi sana ambacho kingekubaliana na maelezo ya unabii huu. Ni Marekani (U.S.A.) peke yake ingeweza kutimiza matarajio hayo.

Lingekuwa jambo jema kama tungekomea papa hapa katika utafiti wetu, lakini tusingeweza kuwa wakweli kwa Maandiko kama tusingesoma maelezo yaliyobaki ya unabii huu. Fungu la kumi na moja na la kumi na mbili yanaendelea kusema hivi, "naye alikuwa na pembe mbili mfano wa mwana-kondoo, akanena kama Joka. Naye atumia uwezo wote wa Mnyama yule wa kwanza mbele yake. Naye aifanya dunia na wote wakaao ndani yake wamsujudie Mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona." Kwa maneno mengine, wakati ungekuja ambapo Marekani ingebadilisha sauti yake ya upole ya kidemokrasia. Chini ya mvuto fulani ingeanza KULAZIMISHA IBADA, "akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia Sanamu yule Mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi. Akapewa kutia pumzi katika ile SANAMU YA MNYAMA, hata ile Sanamu ya Mnyama INENE, na KUWAFANYA wote wasioisujudu Sanamu ya Mnyama WAUAWE. Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, WATIWE CHAPA [ALAMA] katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote ASIWEZE KUNUNUA WALA KUUZA, isipokuwa ana CHAPA [ALAMA] ile, yaani, jina la Mnyama yule, au hesabu ya jina lake." Ufunuo 13:14-17.

Taifa [lo lote] linanena kwa njia ya Sheria zake. Huenda likaonekana kwetu kana kwamba ni jambo lisilosadikika tunaposoma mambo haya leo kwamba [taifa hili la] Marekani lingepata kushawishika kwa kupitisha sheria za dini, na kujaribu KUWALAZIMISHA watu kuabudu kwa mtindo fulani, walakini unabii kamwe haujakosa kutimia. Litaufanyia SANAMU Upapa, au litaanzisha MFUMO UNAOFANANA na mamlaka ile. DINI NA SERIKALI VITAUNGANISHWA pamoja kiasi cha kuweza kulazimisha sheria za dini na kwa njia hiyo litafanana na mfumo ule wa Upapa [wa kuvaa kofia mbili].

Kulingana na unabii huu Amerika mwishowe italazimisha ALAMA YA MNYAMA. Hii inamaanisha nini? Alama yenyewe ni kitu gani? Kwa msingi wa Neno la Mungu tumeonyesha ya kwamba itakuwa ni SABATO YA UONGO [JUMAPILI] ambayo ilianzishwa na Mamlaka ile ya Mnyama [Upapa]. Kule kuitunza Jumapili badala ya Sabato ile ya Biblia kunadaiwa na MAKASISI wake na VIONGOZI kuwa ni kuonyesha UTII kwa Kanisa Katoliki. Je, Marekani baadaye itataka kulazimisha utunzaji wa Jumapili? Hivyo ndivyo hasa mambo yanavyojionyesha sasa hivi katika siasa za Marekani.

Haidhuru tupende kiasi gani kusadiki vinginevyo, nchi yetu hii tuipendayo itaanza kutumia mamlaka yake kulazimisha utunzaji wa Jumapili. Tayari msingi umekwisha kuwekwa. Hivi sasa kila Jimbo (State), isipokuwa moja tu, lina SHERIA ZA JUMAPILI kama hizo katika vitabu vyao. Katika sehemu nyingine [za Majimbo hayo] sheria hizo za dini zimeleta shida kiuchumi kwa Wasabato. Miji mikuu michache imeshurutishwa KUWAKATAZA KUNUNUA AU KUUZA bidhaa zo zote [siku hiyo] kwa wale wanaokataa kuitunza Jumapili. Unabii wa Ufunuo 13:17 unaonyesha kuwa vizuio vya uchumi [kupiga marufuku] vitatumika, "tena kwamba mtu awaye yote ASIWEZE KUNUNUA WALA KUUZA, isipokuwa ana chapa [alama] ile."

 

AMRI YA JUMAPILI KITAIFA IKO KARIBU

Mahakama Kuu ya Marekani (Supreme Court) imekataa kwamba sheria zile za Jumapili [za Majimbo] ni kinyume na KATIBA [ya nchi] ama zina UBAGUZI. Jambo hilo linafungua njia kwa sheria zile za Majimbo ambazo zinaleta utata na ziko kinyume ili ziweze KUBADILISHWA na kuwa SHERIA YA JUMAPILI moja kwa Taifa zima, ambayo itaweka MFUMO MMOJA NA KULAZIMISHA JUMAPILI katika nchi yote ya Amerika. Pamoja na hatua kubwa zinazochukuliwa kuruhusu udhibiti wa Serikali ya Muungano (Federal Control) juu ya uhuru wa mtu mmoja mmoja, hatua hii ya KURATIBU SIKU YA IBADA haitaonekana kuwa ni mapinduzi makubwa sana hapo itakapochukuliwa.

Zingatia haya vizuri: Kutokea kwa mambo hayo kuko upeoni [kumekaribia sana]. Wale wanaokataa kuipokea siku ya uongo ya ibada watakabiliwa na KUTOZWA FAINI, KUZUIWA KUNUNUA NA KUUZA, KIFUNGO, na mwishowe TISHIO LA KIFO. Suala hili la Sabato litakapofanywa hivyo kuwa suala la kitaifa, hapo ndipo watu watakapolazimishwa kukubali kusimama upande mmoja au mwingine. Alama ya Mnyama wakati huo itawekwa juu ya wote WATAKAOKATAA KUITII AMRI YA MUNGU inayowataka kuitakasa Siku ya Sabato. Kwa kuikubali Alama hii ya UTII KWA PAPA [Jumapili], wanaikataa Alama ambayo Mungu anadai kwamba ni ISHARA ya Mamlaka Yake ----- SABATO ya siku ya saba.

 

KUKATA SHAURI

Mmoja anaweza kutoa hoja hii, "Mambo hayo yote yananihusu nini mimi?" Hiyo ni hoja ya maana, na hata jibu lake ni la maana zaidi. Wokovu wako wa milele unategemea UAMUZI wako leo. Huwezi kuutupilia mbali unabii huu unaohusu UTII kwa amri hii ya Sabato. Hakuna hoja juu ya kufaa au kutokufaa kwake. Tunashughulika na Sheria ile ya AMRI KUMI ambayo iliandikwa na Mungu Mwenyewe. Kuvunja mojawapo ya amri hizo ni KUTENDA DHAMBI[Yakobo 2:10-12], na hakuna ye yote anayetenda dhambi kwa makusudi atakayeokolewa. Kuitunza Sabato ya siku ya saba ndicho KIPIMO CHA UTII NA UPENDO kwa Mungu. "Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni DHAMBI." Yakobo 4:17.

Kwa kasi sana ulimwengu huu unajiunga chini [ya mojawapo] ya BENDERA hizo mbili. Wakati UMEKWISHA. Pambano Kuu linafikia hatua zake za mwisho. Wakati ekumenio (ecumenism) inalivuta kundi moja kubwa la madhehebu kuingia katika kambi lisilokuwa na mikazo yo yote ya imani, likiwa limejengwa kabisa juu ya UASI dhidi ya Sabato ya Sheria takatifu ya Mungu, kundi jingine linatambulishwa kuwa ni la wale "wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu." Jaribio hilo kadiri linavyozidi kuwa kali zaidi, ndivyo inavyompasa kila mtu mmoja mmoja KUCHAGUA KUMTII MUNGU au MAPOKEO, KUITUNZA SABATO YA KWELI au ILE YA UONGO [JUMAPILI], KUPOKEA MUHURI WA MUNGU, au ALAMA YA MNYAMA. Sasa ndio wakati wa kulimaliza jambo hili. "Heri wale wazishikao amri zake, wawe na haki kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake." Ufunuo 22:14 (Tafsiri ya Toleo la King James).

The Beast, The Dragon, and The Woman

A dramatic overview of the two contending forces of truth and error as revealed in prophecy.

______________________________________________

by Joe Crews

Mfasiri: M. Mwamalumibili

_____________________________________________

Amazing Facts, Inc.

P.O. Box 1058

Roseville, California 95678-8058

Related Information