SEHEMU YA TATU
Ombi Kwa Wazazi
Waondoeni Watoto Wenu Mbali na Mahali Penye Maovu
Faida yo yote ipatikanayo kutokana na shughuli za kila siku za maisha haya isiruhusiwe kuwashawishi wazazi kuacha kuwalea watoto wao. Kila inapowezekana, ni wajibu wa wazazi kujenga makao yao mashambani [vijijini] kwa ajili ya watoto wao. Watoto na vijana wanapaswa kulindwa kwa uangalifu. Wangeondolewa na kupelekwa mbali na mahali penye maovu mengi ambapo panapatikana katika miji yetu. Hebu na wazungushiwe mivuto ile inayopatikana katika nyumba ya kweli ya Kikristo ----- yaani, nyumba ile anamokaa Kristo. ----- Letter 268, 1906.
Kabla Pigo Lile Halijafurika
Kabla pigo lile halijafurika juu ya wakazi wa dunia hii, Bwana anawaagiza wale walio Waisraeli kweli kweli kujiweka tayari kwa tukio lile. Kwa wazazi anawapelekea kilio cha onyo, akisema, Wakusanyeni watoto wenu na kuwaleta nyumbani mwenu; wakusanyeni na kuwatenga mbali na wale wanaozidharau amri [kumi] za Mungu, yaani, wale wanaofundisha watu uovu na kutenda uovu. Tokeni nje ya miji mikubwa haraka iwezekanavyo. Jengeni shule zinazoendeshwa na kanisa. Wapeni watoto wenu Neno la Mungu kama msingi wa elimu yao yote. ----- Testimonies, Gombo la 6, uk. 195.
Nimeagizwa na Bwana niwaonye watu wetu wasikimbilie kwa wingi mijini ili kujijengea makazi humo kwa ajili ya familia zao. Kwa akina baba na akina mama nimeagizwa kusema maneno haya, Msikose kuwatunza watoto wenu ili wabaki ndani ya maeneo ya nyumba na viwanja vyenu. ----- Manuscript 81, 1900.
Roho za Watoto Wenu au Maisha Rahisi na Starehe Zenu
Ninyi msiendelee tena kuwaweka watoto wenu mahali pale watakapokabiliana na majaribu yaliyomo mijini, miji ambayo imefikia kilele chake cha kuangamizwa. Bwana ametuma onyo lake kwetu pamoja na ushauri wake ili tutoke mijini. Basi na tusiendelee kuweka vitega uchumi zaidi katika miji hiyo. Akina baba na mama, mnazifikiriaje roho za watoto wenu? Je! mnawatayarisha waliomo nyumbani mwenu kwa kunyakuliwa kwenda katika majumba yale ya kifalme kule mbinguni? Je! mnawaandaa hao kuwa miongoni mwa familia ile ya kifalme? yaani, watoto wa Mfalme yule wa mbinguni? "Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake?" [Mathayo 16:26.] Mtalinganishaje maisha rahisi, starehe,hali ile yenye manufaa isiyo na wasiwasi [iliyomo humo mijini] na thamani ya roho za watoto wenu? ----- Manuscript 76, 1905.
Tabia za Kikristo Zinajengeka Vizuri Zaidi Katika Maeneo ya Upweke
Hakuna hata familia moja katika mia ambayo ikiendelea kukaa mjini itakuwa na maendeleo mazuri kimwili, kiakili, au kiroho. Imani, tumaini, upendo, furaha, vinaweza kupatikana kwa vizuri zaidi katika mahali pa upweke, ambapo pana mashamba na vilima na miti. Nendeni na watoto wenu mbali na mambo yale yanayoonekana waziwazi [tamasha] na sauti za mjini, mbali na makelele ya magari yanayopita mitaani pamoja na makundi ya watu, hapo ndipo akili zao [watoto wenu] zitakuwa na afya zaidi. Itaonekana kuwa ni rahisi zaidi kwao kuikumbuka mioyoni mwao kweli ile ya Neno la Mungu. ----- Manuscript 76, 1905.
Wapelekeni watoto wenu kwenye shule zile zilizomo mjini, ambako kila aina ya majaribu huwangojea ili kuwatamanisha na kuwadhalilisha, ndipo kazi ile ya kujenga tabia itakuwa ngumu mara kumi kwa pande zote mbili, yaani, kwa wazazi na kwa watoto. ----- Fundamentals of Christian Education, uk. 326. (1894)
Kimbilio Katika Maeneo ya Mashambani
Wazazi na waelewe ya kwamba malezi ya watoto wao ni kazi ya maana katika kuziokoa roho zao. Katika maeneo yale ya mashambani [vijijini] mazoezi ya viungo mengi ya kufanya yenye manufaa [kiafya] yatapatikana kwa kufanya mambo yale yanayopaswa kufanywa, ambayo yatawapa afya ya kimwili kwa kuzikuza neva zao na misuli. Tokeni mijini, huo ndio ujumbe wangu kwa ajili ya kuwalea watoto wetu katika maadili mema.
Mungu aliwapa wazazi wetu wale wa kwanza njia ya elimu ya kweli alipowaagiza kuilima ardhi na kuyatunza makao yao katika Bustani ile. Baada ya dhambi kuingia, kutokana na utovu wao wa utii kwa matakwa yake Bwana, kazi iliyofanyika kuilima ardhi ikawa imeongezeka sana, maana nchi, kutokana na laana ile, ikazaa magugu na michongoma. Lakini kazi ile yenyewe haikutolewa kwao kwa sababu ya dhambi. Bwana Mkuu Mwenyewe akaibarikia kazi ile ya kuilima ardhi.
"KAMA VILE ILIVYOKUWA ... SIKU ZA NUHU"
Ni kusudi lake Shetani kuwashawishi wanaume na wanawake kwenda mijini, isitoshe, ili kufikia lengo lake anavumbua kila namna ya mambo mapya [mitindo mipya] na burudani, kila aina ya mambo ya kusisimua. Na miji ya ulimwengu wa leo inageuka na kuwa kama ilivyokuwa miji ile kabla ya Gharika.
Daima tungebeba mzigo huo [wa kujihadhari] tunapoyaona maneno hayo ya Kristo yakitimia, "Kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu." Mathayo 24:37. Katika siku zile kabla ya Gharika, kila aina ya burudani ilibuniwa ili kuwafanya wanaume na wanawake kuwa na usahaulifu [wa mambo ya Mungu] na kutenda dhambi. Leo hii, mwaka huu wa 1908, Shetani anafanya kazi yake kwa nguvu nyingi, ili hali zile zile zipate kuwapo. Nao ulimwengu unazidi kuwa mwovu. Uhuru wa dini hautaheshimiwa sana na wale wanaojiita Wakristo, kwa kuwa wengi wao hawayajui kabisa mambo ya kiroho.
Hatuwezi kushindwa kuona ya kwamba mwisho wa ulimwengu huu karibu sana unakuja. Shetani anafanya kazi yake katika mioyo [mawazo] ya wanaume na wanawake, na wengi wanaonekana kana kwamba wamejazwa na tamaa ya kupata burudani na misisimko. Kama vile ilivyokuwa katika siku zile za Nuhu, kila aina ya uovu inazidi kuongezeka. Kwa wakati kama huu, watu wale wanaojaribu kuzishika amri [kumi] za Mungu wangetafuta mahali pa upweke [pa kuishi] mbali na miji hiyo....
SI HASARA KWENU
Ni nani basi atakayeonywa? Tunarudia tena kusema, Tokeni Mijini. Msidhani kwamba ni hasara kubwa sana kwenu, kwamba ni lazima kwenda vilimani na milimani, bali tafuteni mahali pale pa upweke [ukimya] ambapo mnaweza kuwa na Mungu peke yenu, mkijifunza mapenzi yake na njia yake....
Ninawasihi watu wetu kuifanya iwe ndiyo kazi yao ya maisha kutafuta maisha yao ya kiroho. Kristo yu mlangoni. Hii ndiyo maana nawaambia watu wetu, Msifikirie ya kuwa ni taabu mnapoitwa kuiacha miji na kuhamia katika maeneo ya shamba [vijijini]. Huko mibaraka mingi inawangojea wale watakaoishikilia. Kwa kuziangalia mandhari zile [sura za nchi] za maumbile, yaani, kazi ile ya Muumbaji, kwa kujifunza kazi ya mikono yake [uumbaji wake] Mungu, bila kujitambua mtabadilishwa na kufanana naye. ----- Manuscript 85, 1908.
Kujipatia Matunda Bora Kabisa ya Maisha Haya
Jengo la gharama nyingi, fanicha iliyonakishiwa sana, mapambo, anasa, na raha, mambo hayo hayaleti hali zile zilizo za muhimu kwa maisha ya furaha, yenye manufaa. Yesu alikuja hapa duniani kufanya kazi kubwa sana iliyopata kufanywa miongoni mwa wanadamu. Alikuja kama balozi [mjumbe] wa Mungu, kutuonyesha sisi jinsi ya kuishi ili tuweze kujipatia matunda bora kabisa ya maisha haya. Ni hali [mazingira] gani basi zilizochaguliwa na Baba yetu wa milele kwa ajili ya Mwanawe? Ni nyumba ile iliyokaa mahali pale pa upweke [kimya] katika vilima vile vya Galilaya; nyumba iliyopata mahitaji yake kwa kazi ya uaminifu, yenye heshima; maisha yale ya kawaida; kupambana kila siku na matatizo pamoja na shida; kujikana nafsi, matumizi mazuri ya kipato chao, na huduma yao iliyotolewa kwa moyo wa uvumilivu na furaha; saa ile ya kujifunza kando ya mama yake, wakiwa na gombo la Maandiko lililofunguliwa wazi; macheo yale tulivu au utusitusi ule wa asubuhi katika bonde lile la majani mabichi; huduma takatifu ya maumbile yale; kujifunza uumbaji na maongozi ya Mungu; na moyo wake kuwasiliana na Mungu, ----- hizo zilikuwa ndizo hali [mazingira] na nafasi nzuri za maisha ya mwanzo ya Yesu
WAKUU NI URITHI UTOKANAO NA MAISHA YA SHAMBA
Hivyo ndivyo ilivyo kwa sehemu kubwa ya watu walio bora na wakuu katika vizazi vyote. Someni historia ya Ibrahimu, Yakobo, na Yusufu, na ya Musa, Daudi, na Elisha. Jifunzeni maisha ya watu wa nyakati zilizofuata baadaye waliostahili kabisa kuzijaza nafasi zile za amana na madaraka, watu ambao mvuto wao umekuwa na mafanikio makubwa sana katika kuuinua juu ulimwengu huu.
Ni wangapi miongoni mwa hao walilelewa katika makazi ya mashambani [vijijini]. Hawakuijua anasa hata kidogo. Hawakuutumia ujana wao katika burudani. Wengi walilazimika kupigana na umaskini na shida. Walijifunza mapema kufanya kazi [kwa mikono yao], na maisha yao ya kujishughulisha sana katika maeneo yale yaliyo wazi yaliwapa nguvu za kimwili na kupanuka kwa uwezo wao kiakili. Wakiwa wamelazimika kutegemea rasilimali [nyenzo] zile walizokuwa nazo, walijifunza kupambana na shida na kuvishinda vipingamizi, tena walijipatia ujasiri na uvumilivu. Walijifunza masomo ya kujitegemea na kujitawala nafsi zao. Wakiwa wamekingwa kwa kiwango kikubwa mbali na marafiki wabaya, walitosheka na furaha za kawaida na urafiki mzuri ujengao. Katika uchu wao wa chakula walifuata chakula cha kawaida na kuwa na kiasi katika mazoea yao. Walitawaliwa na kanuni, tena walikua wakiwa safi [wakiwa na mwenendo mzuri], wakiwa na nguvu na unyofu wa moyo. Walipotakiwa kufanya kazi zao za maisha, walikwenda wakiwa na nguvu za kimwili na kiakili, wakiwa na moyo uliochangamka, na uwezo wa kupanga mipango na kuitekeleza, tena wakiwa na uthabiti wa kuyapinga maovu, mambo ambayo yaliwafanya kuwa na uwezo dhahiri wa kutenda mema ulimwenguni.
BORA KULIKO UTAJIRI
Bora kuliko urithi mwingine wo wote mnaoweza kuwapa watoto wenu itakuwa ni zawadi ile mtakayowapa ya mwili wenye afya, akili timamu, na tabia nzuri. Wale wanaojua kile kinacholeta ufanisi wa kweli katika maisha haya mara nyingine watakuwa na busara. Wataweka mbele yao mambo yale yaliyo bora kwa namna watakavyochagua makazi yao.
Badala ya kuishi mahali pale ambapo kazi za wanadamu zinaweza kuonekana waziwazi, penye tamasha na sauti zinazoamsha mawazo machafu, mahali pale ambapo misukosuko na ghasia huleta uchovu na wasiwasi, nendeni mahali ambako mnaweza kuangalia kazi za [uumbaji wa] Mungu. Jipatieni pumziko la nafsi zenu katika uzuri na utulivu na amani ya maumbile [viumbe vya asili]. Jicho lenu na liangalie mashamba ya chanikiwiti, vijisitu, pamoja na vilima. Angalieni mbingu ile ya samawi, isiyozuiwa na vumbi na moshi wa mjini hata isiweze kuonekana, vuteni hewa ile ya mbinguni inayowatia nguvu. Mbali na mambo yale yaliyomo mjini yanayovuta mawazo yenu na kuyatawanya, nendeni pale mnapoweza kukaa kirafiki na watoto wenu, mnapoweza kuwafundisha ili wapate kujifunza habari za Mungu kwa njia ya kazi zake [uumbaji wake], na kuwalea ili wawe na maisha ya unyofu na yenye manufaa [kwao wenyewe na kwa wengine]. ----- The Ministry of Healing, uk. 265-267. (1905)
Faida Nyingi za Shughuli Zinazofanyika Nje
Lingekuwa ni jambo jema kwenu kuweka kando masumbufu yenu yanayowafadhaisha, na kupata mahali pa faragha huko shamba [vijijini], ambako hakuna mvuto wenye nguvu wa kuyaharibu maadili ya watoto na vijana wenu.
Ni kweli, hamtaweza kuondokana kabisa na maudhi yote pamoja na masumbufu yanayofadhaisha; lakini kule mgeweza kuyaepuka maovu mengi na kufunga mlango dhidi ya gharika ya majaribu yanayotishia kuyatawala kabisa mawazo ya watoto wenu. Wanahitaji kazi ya kufanya na mambo mbalimbali tofauti ya kushughulika nayo. Mambo ya jinsi ile ile waliyozoea kufanya nyumbani mwenu huwafanya wasiwe na raha [huwakinai], na kuwa watukutu, kisha wanajiingiza katika tabia ile ya kujichanganya pamoja na vijana wale waovu wa mjini, hivyo hujipatia elimu ya mitaani huko....
Kuishi huko shamba [vijijini] kungewaletea [watoto na vijana] manufaa mengi sana; maisha yao ya shughuli nyingi nje ya nyumba yangekuza afya yao kiakili na kimwili. Wawe na bustani ya kupalilia, ambamo watapata furaha na kazi yenye manufaa kwao. Kuitunza mimea na maua kuna mwelekeo wa kukuza akili za kupambanua mema na mabaya pamoja na kuwa na busara, na wakati uo huo ufahamu wao kuhusu uumbaji mzuri na wenye manufaa wa Mungu una mvuto kwao unaowabadilisha na kuwafanya wawe waungwana katika mawazo yao, wakiuhusisha [uumbaji huo] na Muumbaji na Bwana huyo wa vyote. ----- Testimonies, Gombo la 4, uk. 136. (1876)
Tusitazamie Mwujiza Wo Wote Kuigeuza Njia Yetu Mbaya
Nayaangalia maua haya, na kila wakati ninapoyaangalia nafikiria juu ya Edeni. Hayo yanaonyesha upendo wa Mungu alio nao kwetu. Hivyo anatupatia sisi katika dunia hii mwonjo mdogo tu wa Edeni ile. Anatutaka sisi kufurahia vitu vizuri alivyoviumba, na ndani yake kuona sura [picha] ya kile anachotaka kutufanyia sisi.
Anatutaka sisi kuishi mahali pale palipo na nafasi tele. Watu wake hawatakiwi kusongamana mijini. Anawataka waende na familia zao nje ya miji, ili wapate kujiandaa vizuri kwa ajili ya uzima ule wa milele. Kitambo kidogo [kilichobaki] watalazimika kuondoka mijini.
Miji hiyo imejaa uovu wa kila namna, ----- pamoja na migomo na mauaji na watu kujiua wenyewe. Shetani yu ndani yake [miji hiyo], akiwaongoza watu katika kazi yao ya maangamizi. Chini ya mvuto wake wanaua kwa sababu tu ya kuua, na kitendo hicho wataendelea zaidi na zaidi kufanya....
Tukijiweka wenyewe chini ya mivuto ile mibaya iliyokatazwa, je! tutazamie kwamba Mungu atafanya mwujiza wo wote wa kuigeuza njia yetu hiyo mbaya? ----- La, hasha. Tokeni mijini haraka iwezekanavyo, na kununua sehemu ndogo ya ardhi [vijijini], ambako mnaweza kuwa na bustani, mahali ambako watoto wenu wanaweza kuyaangalia maua yakuapo, na kujifunza kwayo mafunzo ya kuwa na maisha ya kawaida na usafi wa moyo. ----- General Conference Bulletin, Machi 30, 1903.