>Mwanzo >Soma vitabu >SURA YA KWANZA >SURA YA PILI

SURA YA PILI

II. J O K A N A M W A N A M K E

 

Kufikia hapa tuko tayari kuuliza swali jingine kuhusu kujitwalia mamlaka kwa upande wa Mnyama huyu. Alipokea kwa nani uwezo wa kuitawala dunia kwa miaka ile 1260, na kuwatesa mamilioni [ya watakatifu aliowaita wazushi] kiasi hicho kwa ajili ya imani yao? Jibu linapatikana katika Ufunuo 13:2, "yule Joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi." Angalia ya kwamba MAMLAKA yake inatoka kwa JOKA. Lakini Joka huyu ni nani? Ufunuo 12:7-9: "Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule Joka, yule Joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule Joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye."

Joka ni Shetani mwenyewe hasa. Lakini ni lini Shetani alipoudanganya ulimwengu wote? Alipotupwa chini kutoka mbinguni palikuwa na watu wawili tu duniani, na hao ndio walioiwakilisha dunia yote. Kwa kuwadanganya Adamu na Hawa katika Bustani ile ya Edeni, Shetani aliifanya dunia yote ipotee, naye akaimiliki kwa muda. PAMBANO KUU kati ya mema na mabaya, ambalo lilianza kule mbinguni, sasa likawa limehamia katika sayari hii.

 

UTABIRI WA UADUI

Baada ya anguko la mwanadamu Mungu alitamka laana juu ya kila mshiriki katika kosa lile la kwanza. Katika Mwanzo 3:15, tunasoma juu ya laana ambayo iliwekwa juu ya Mwovu au Joka. "Nami nitaweka UADUI kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino." Hapa kuna unabii wa pambano hili lililodumu kwa vizazi vyote ambalo lingekuwapo kati ya Joka na Mwanamke, kati ya uzao wa Joka na uzao wa Mwanamke.

Lakini Mwanamke huyu aliyetajwa katika unabii huu ni nani? Mwanamke, katika unabii wa Biblia, sikuzote analiwakilisha Kanisa. Katika Yeremia 6:2 tunasoma hivi, "Nimemlinganisha Binti Sayuni na mwanamke aliye mzuri, mwororo." [Tafsiri ya King James Version]. Sayuni ni nani? Isaya 51:16, "na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu." Kwa hiyo, pambano hilo kuu limekuwa likiendelea tangu Edeni. Kumekuwa na pande mbili tu tangu wakati ule mpaka sasa. Joka na wafuasi wake wamejipanga dhidi ya Mungu na wafuasi Wake. Kweli dhidi ya Uongo, na Shetani dhidi ya Kanisa.

 

 PANDE MBILI

Shetani na Mungu wamekuwa wakishindania kumtawala kila mwanadamu aliye hai. Hata katika wana wa Adamu pande hizo mbili ziliwakilishwa. Kaini alikuwa upande wa Joka, naye alitaka kuweka njia yake mwenyewe badala ya njia ya Mungu aliyokuwa amemwamuru. Habili alikuwa upande wa Mungu, naye alikuwa mwenye haki sana hata Kaini akamwua hatimaye. Je, unakumbuka Mungu alivyomwambia kila mmoja wao kuleta mwana kondoo, lakini Kaini akaleta matunda na mboga za majani badala ya kile Mungu alichokuwa amewaagiza kuleta kama kafara [dhabihu]? Utagundua kwamba sikuzote hiyo itakuwa ndiyo ALAMA ya Joka. Anajaribu kuweka kitu kingine badala yake au kuleta kitu cha bandia na kukiweka mahali pa kweli halisi ya Mungu.

Katika vizazi vyote vya Kaini dunia ilikuwa imeharibika sana hata Mungu akalazimika kuiangamiza kwa Gharika. Lakini baada ya Gharika pande mbili tena zikaonekana. Wafuasi wa Joka wakakaa kwa wingi katika mji wa Babeli, nao wakajaribu kumchokoza Mungu kwa kujenga mnara mrefu ambao ungefika mbinguni. Kwa kweli mpango ule ulishindikana, na eneo lile la mnara ule wa Babeli baadaye likawa mji wa Babeli (Babylon), ambao, katika mwaka wa 606 K.K. ulianza kutawala kama Dola ya kwanza ya ulimwengu mzima.

Katika miaka ile ya mwanzo ya machafuko Mungu alimwita Ibrahimu kutoka Babeli, na kumtuma Kanaani. Ibrahimu alikuwa amekulia [katika mji ule wa Babeli] kule Mesopotamia, karibu na mahali ambapo mnara ule mrefu wa Babeli ulijaribiwa kujengwa, na mahali ambapo dola ile ya Babeli ilianzishwa. Siku zote mpango wa Mungu umeambatana na mwito wa kujitenga na MACHAFUKO YA UONGO.

 

 JOKA NA IBADA YA JUA

Hebu na tujifunze historia inayohusu upande wa Joka kwa kifupi. Mfumo wa kipagani wa dini ulianzia pale [Babeli] katika mtindo ule wa KUABUDU JUA. Ilikuwa ni ibada ya sanamu ya kumkashifu Mungu, iliyojaa ufisadi, sherehe za ukware [uasherati], na ibada za aibu. Lakini kitambo kidogo tu wafuasi wale wa Joka wakaanza kugombana wao kwa wao na Umedi-Uajemi ikatwaa mamlaka. Ibada ya Baali ikaendelea na kukithiri kama ilivyokuwa katika ufalme uliotangulia. Ndipo Uyunani ikatwaa mamlaka, lakini nayo ikachangia katika kuendeleza ibada iyo hiyo ya jua. Mwishowe, Rumi ikaanza kutawala ulimwengu. Walakini hapakuwa na badiliko lo lote katika dini. Umithra (Mithraism), au IBADA YA JUA, ulikuwa ndiyo dini ya ulimwengu wote wa Dola ile ya Kipagani ya Rumi. Toka Babeli mpaka Rumi, Joka alitawala kwa njia ya ibada ya jua ya kishenzi [kipagani].

Lakini wakati wa utawala wa Warumi, jambo kubwa lilitokea! Ulikuwa ni wakati wa uzao wa mwanamke kutokea! Kumbuka, ya kwamba unabii ulizungumzia juu ya uadui kati ya uzao wa Mwanamke na uzao wa Joka. Uzao wa Mwanamke ulitokea katika siku za Dola ya Kirumi. Hebu na tusome habari zake katika Ufunuo 12:1, "Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili." Usisahau kwamba Mwanamke katika unabii anawakilisha Kanisa. Mwanamke Safi anawakilisha Kanisa la Kweli [la Mungu], lakini Mwanamke Kahaba anawakilisha mfumo wa Dini ya Uongo [Kanisa lililomwasi Mungu].

 

MZAO WA MWANAMKE

Mwanamke huyu aliyevaa mavazi meupe, aliyeelezwa katika Ufunuo kumi na mbili, analiwakilisha Kanisa la kweli, Kanisa la Mitume, lenye mafundisho safi ya dini. Nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake ni Mitume wale kumi na wawili. "Naye alikuwa na mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa. Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba [taji] saba. Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake. Naye akazaa mtoto manamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi." Ufunuo 12:2-5. Sasa, basi, mtoto huyo mwanamume alikuwa ni nani? Pamekuwapo na mtoto mwanamume mmoja tu aliyekusudiwa kuyatawala mataifa yote na ambaye alinyakuliwa hata kwenye kiti cha enzi cha Mungu. Alikuwa si mwingine bali ni Yesu Kristo. Lakini ni nani aliyejaribu kumwua mtoto huyo mara tu baada ya kuzaliwa kwake? Unajibu, Ni Herode, mfalme wa Kirumi." Na hivyo ndivyo ilivyokuwa hasa. Herode alijaribu kuwaua watoto wote wa kiume katika nchi ile ya Yudea, kwa jitihada ya kumwangamiza Kristo.

Kwa hiyo, Dola ya Kirumi inawakilishwa katika unabii wa Biblia na Joka lile lile kama alivyo Ibilisi mwenyewe. Kwa vile Shetani alifanya kazi yake kwa karibu sana kupitia kwa taifa lile ili kumwangamiza Yesu, Rumi ya Kipagani nayo inawakilishwa na mfano ule ule [wa Joka Jekundu] katika unabii huu kama [anavyowakiliswa] Ibilisi. Walakini Herode hakufanikiwa katika jaribio lake la kumwangamiza mtoto yule mwanamume. Mariamu na Yusufu wakakimbilia Misri na kuokoka kutokana na amri ile ya kutisha. Pigo la kifo la Shetani la kumwangamiza Yesu pale msalabani lilishindwa siku ile ya Jumapili asubuhi wakati Yule Aliyesulibiwa alipovivunja vifungo vya mauti kwa njia ya ufufuo ule. Siku arobaini baadaye alinyakuliwa hata mbinguni kwa utimilizo mkamilifu wa maneno ya unabii huu.

Joka alipoona ya kuwa hakuwa na uwezo wa kumwangamiza Kristo, aligeuza ghadhabu yake dhidi ya Kanisa lile la mwanzo. Kwa mujibu wa Ufunuo 12:13, "Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi [alimtesa] mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume." Wakati ule ilikuwapo idadi ndogo tu ya Wakristo katika ulimwengu wote, na Shetani alijisikia ya kwamba angeweza kuwafutilia mbali kabisa kwa mateso. Maelfu kwa maelfu ya Wakristo waliuawa chini ya mateso yale ya kutisha yaliyoendeshwa na Wafalme wakatili wa Kirumi. Lakini Injili ilizidi kukua na kuenea mahali pengi. Damu ya wafia dini wale ilionekana kuwa ni mbegu ya Kanisa. Alipokufa mmoja waliinuka mia moja zaidi kuijaza nafasi yake. Paulo alihubiri Injili yake mpaka milangoni mwa Rumi. Joka yule wa zamani akaingiwa na wasiwasi. Huo haukuwa ni wakati unaofaa kwa uzao wa Joka kuonekana.

 

UZAO WA JOKA

Kwa karne nyingi Shetani alijitahidi kuwaangamiza watu wa Mungu kwa kutumia upinzani wa kikatili wa Babeli, Umedi-Uajemi, Uyunani, na Rumi. Kwa njia ya ukatili sana na mateso alikuwa ameshindwa kuifutilia mbali ile kweli [Neno la Mungu]. Basi, kile alichokuwa hana uwezo kufanya kwa kutumia nguvu, Joka sasa angejaribu kufanya kwa kutumia mbinu na udanganyifu. Angeanzisha MFUMO WAKE WA DINI BANDIA[YA UONGO]. Angeingiza mafundisho ya dini ya kipagani na falsafa kutoka katika Dola zile za zamani za Babeli, Umedi-Uajemi, Uyunani na Rumi, na kuyachanganya pamoja na mafundisho ya dini ya Kikristo. Kwa njia hiyo, alijitahidi kuwaangamiza mamilioni kwa udanganyifu wake.

Katika umbile gani uzao huu wa Joka ulitokea? Uliletwa kwa mfano wa Mnyama yule wa Ufunuo 13. Ni jambo la maana sana ya kwamba Mnyama huyo ameumbwa kwa sehemu za simba, chui, dubu, na mnyama wa kutisha asiyekuwa na jina wa Danieli 7. Picha [katuni] hii ya UPAPA aliyoitoa Mungu inatudhihirishia ya kuwa [Mnyama huyo] aliumbwa kwa sehemu zinazotokana na falme zile zote za zamani za kipagani. Hasa alipata nguvu zake kutoka kwa taifa lile la kipagani la Rumi. Kwa mujibu wa Ufunuo 13:2, Joka alimpa Mnyama huyo nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. Tumejifunza ya kwamba Joka huyo anaiwakilisha hasa Dola ya Kipagani ya Rumi, pamoja na kumwakilisha Shetani mwenyewe.

Je, Dola ya Kipagani ya Rumi ilipata kuupa mamlaka yo yote Upapa? Ukweli ni huu, kwamba katika mwaka ule wa 330 B.K. Konstantino (Constantine), Mfalme wa Rumi, aliukabidhi mji wote wa Rumi kwa Papa kama kiti chake cha enzi. Historia inatumia karibu maneno yale yale ya unabii huu katika kukielezea kitendo hicho. Nitanukuu kutoka kwenye chanzo kimoja cha Kikatoliki na kutoka katika kitabu kimoja cha historia. "Dola ya Rumi ilipogeuka na kuwa ya Kikristo, na amani ilipohakikishwa mfalme [Konstantino] aliiacha Rumi mikononi mwa Papa, kuwa kiti cha mamlaka yake yule Aliye Badala ya Kristo (Vicar of Christ), ambaye angetawala mle akiwa haingiliwi na mamlaka yo yote ya kibinadamu, mpaka mwisho wa dahari, mpaka mwisho wa wakati." PAPAL RIGHTS AND PRIVILEGES, uk.13,14.

"Uhamishaji wa makao makuu ya dola kutoka Rumi kwenda Konstantinopo (Constantinople) katika mwaka ule wa 330 B.K., uliliacha Kanisa lile la Magharibi [Upapa] kuwa huru kabisa mbali na mamlaka yo yote ya kifalme, kuuendeleza mfumo wake wa utawala. Askofu wa Rumi [Papa], akiwa amekikalia kiti chake cha enzi cha Makaisari, kwa sasa akawa mtu mkubwa sana katika eneo la [Ulaya] Magharibi, na kitambo kidogo tu baadaye akalazimika kuwa KIONGOZI WA KISIASA na pia kuwa KIONGOZI WA KIROHO." THE RISE OF THE MEDIEVAL CHURCH, ukurasa 168. Ni kwa wazi jinsi gani semi hizi [mbili] huonyesha kwamba Upapa ulipokea kiti chake cha enzi na uwezo kutoka kwa Rumi ya Kipagani! Lakini Rumi iliupata wapi? Toka kwa Uyunani. Na Uyunani iliupata wapi uwezo wake? Toka kwa Umedi-Uajemi. Na Umedi-Uajemi iliupata wake wapi? Toka kwa Babeli. Na Babeli iliupata wapi? Toka kwa yule Joka. Basi, tunaanza kuelewa kwa nini Mungu ametoa maonyo ya kutisha kama hayo dhidi ya mamlaka hii ya Mnyama. Joka yuko nyuma yake kabisa.

 

MADANGANYO KATIKA VAZI LA KIPAGANI

Hebu na tutafakari kwa dakika chache jinsi mafundisho ya dini ya kipagani yalivyoweza kupata nafasi ya kuingia katika mfumo huo wa dini ya bandia [uongo] ambayo Shetani aliianzisha. Kwa sababu dalili ya uwezo wa Joka ni kudanganya kwa KUIGIZA na kuweka kitu kingine mahali pa kile kilichokuwapo, basi, tutaweza kuona katika mfumo huo wa KIDINI-KISIASA utendaji wake Shetani akitumia juhudi yake yote ya kishetani. Kama ilivyokuwa katika suala lile la Kaini, vitu vya badala viliwekwa [mahali pa vyenyewe] ili kutimiza amri za Mungu. Kumbukumbu (relics) nyingi za ibada ya jua zilikuja kupewa cheo cha Kikristo. Seti nzima ya mafundisho ya uongo iliongezwa ili Upapa uweze kupata fahari kubwa kwa watu wale wapagani wa kizazi kile. Sanamu za kipagani zikaachwa mlangoni [mwa kanisa], lakini sanamu za Petro, Maria na watakatifu zikachukua mahali pao.

Kama kielelezo hai cha njia zilizofanya dhana za kipagani kuingia kanisani, hebu fikiria mfano wa Krismasi. Je, unajua usherehekeaji wa Krismasi ulikoanzia? Krismasi, kama sikukuu, ilikuwako muda mrefu sana kabla ya Yesu kuzaliwa duniani humu. Desemba ishirini na tano, kwa kweli, ilisherehekewa mamia ya miaka kabla ya kuzaliwa Kristo. Wapagani waliliabudu jua, nao wakagundua ya kwamba katika mwezi ule wa Desemba siku zilikuwa zinazidi kuwa fupi na fupi zaidi, na jua lilikuwa linakwenda mbali sana kutoka kwao. Wakiwa wamejawa na hofu kwamba jua lingeweza kuwaacha kabisa, wakaanza kusali na kutoa sadaka. Kisha tarehe ishirini na tano Desemba, kwa mara ya kwanza, waliweza kujua ya kwamba jua lilikuwa linarudi kwao kwa karibu zaidi; siku zilikuwa zinaanza kuwa ndefu tena. Basi, watu hao wakasema, "Jua limezaliwa upya kwetu." Wakaiita tarehe ishirini na tano ya Desemba kuwa ni SIKU YA KUZALIWA JUA, ama MUNGU-JUA. Ikawa ni SIKUKUU KUBWA SANA ya kidini kwao.

Siku ile ilisherehekewa na wapagani peke yao mpaka mfumo huo bandia wa Upapa ulipoanza kujitokeza. Wakati ule siku ile ikachaguliwa na Upapa na kuanza kutumika, nayo ikaitwa SIKU YA KUZALIWA MWANA (S-O-N), badala ya SIKU YA KUZALIWA JUA (S-U-N). Dkt. Gilbert Murray, M.A., D. Litt., LL.D., F.B.A., profesa wa Lugha ya Kigiriki katika Chuo Kikuu cha Oxford, ameandika haya: "Umithra (Mithraism) ulikubalika sana, hata ukaweza kuulazimisha ulimwengu ule wa Kikristo kuweka siku yake ya jua (Sun-day) mahali pa [siku ya] Sabato; na sikukuu yake ya kuzaliwa jua, tarehe 25 Desemba, kuwa ndiyo siku ya kuzaliwa Yesu." HISTORY OF CHRISTIANITY IN THE LIGHT OF MODERN KNOWLEDGE, Sura ya III; yamedondolewa kutoka katika kitabu cha "RELIGION AND PHILOSOPHY," uk.73,74. New York: 1929.

Kwa kweli, hatuijui tarehe ya kuzaliwa kwake Kristo. Kama unavyoweza kuona bila shida, kuitumia tarehe ishirini na tano ya Desemba kulijengwa kabisa juu ya maadhimisho ya sikukuu ile ya kuabudu jua. Tafadhali zingatia jinsi siku hii iliyowekwa na wapagani inavyoweza kuteleza kirahisi na kuingia katika makanisa ya Kikristo, na hata inaweza kurithiwa [kupokewa] na Uprotestanti.

Ni vipi kuhusu Pasaka (Easter)? Ni sherehe inayojulikana sana ambayo inaadhimishwa na makanisa yetu ya siku hizi. Walakini hii pia ilisherehekewa na wapagani muda mrefu kabla ya ufufuo wa Kristo. Makundi yote ya Wakristo wanagundua kwamba Jumapili ya Pasaka mara nyingi inahitilafiana kwa umbali wa majuma matano toka mwaka mmoja kwenda mwaka mwingine. Wachache wanajua kwamba inatawaliwa na mianga ile ya mbinguni. Siku zote Pasaka inaangukia Jumapili ya kwanza baada ya mwezi mpevu (full moon) mara tu baada ya jua kuwa kichwani kaskazini ya Ikweta (Equinox ----- March 2l).

Wapagani wale wa zamani za kale waligundua ya kwamba kila kitu kilionekana kupata uzima mpya mapema katika majira yale ya kuchipua (Spring), mara tu baada ya jua kupita mstari wa ikwinoksi (equinox) kaskazini ya Ikweta. Basi wakachagua siku moja katika majira ya kuchipua [Machi, Aprili, Mei] ili kumheshimu mungu wa kike wa uzazi. Siku ile ikatolewa kwa ISHTA (ISHTAR), mungu wa kike wa uzazi, kwa sababu ya uhai mpya na kukua kwa mimea ya asili. Neno lilo hilo ISTA (EASTER) limeandikwa kwa herufi nyingine zisizokuwa za lugha yenyewe kutokana na jina la mungu huyo wa kike ISHTA (ISHTAR), ambaye ibada yake iliwekewa ukumbusho wake kwa kutumia sikukuu ya Ista (Easter) [Pasaka].

Mara nyingi Wakristo walei [wa kawaida] wameuliza ya kwamba ule mkate mdogo kama sungura (bunny rabbit) na yai la Ista (Easter egg) vina uhusiano gani na ufufuo wa Kristo. Kusema kweli, havina uhusiano wo wote na [ufufuo] huo. Sungura alichaguliwa kwa sababu alikuwa anazaa sana. Yai pia lilichaguliwa kwa sababu lilikuwa nembo ya kuzaa sana. Hata nembo hizo zenyewe, mkate mdogo kama sungura na mayai, vinatunzwa kama ukumbusho wa asili yake ya kipagani [ya siku hiyo]. Mifano hii imetolewa ili kuonyesha tu jinsi ilivyokuwa rahisi kwa Mwovu kulazimisha mawazo yale ya kipagani juu ya kanisa lile. Upapa ulipotokea ulikuwa uko tayari kuzipokea desturi zile zisizoungwa mkono na Biblia ambazo ziliashiria kwa wazi ya kwamba [mfumo] huo ulikuwa ndiyo ile mamlaka kuu ya bandia iliyoelezwa na Mungu katika Ufunuo 13.

Kufikia hapa swali linakuja mawazoni mwetu, ----- Hivi ni kweli tunaifuata Biblia katika mafundisho yetu yote ya dini? Iwapo MAPOKEO na DESTURI za kipagani zimeweza kuteleza kwa urahisi na kuingia kanisani, ni vipi kuhusu mafundisho mengine ya dini? Mpaka sasa mambo yaliyokwisha kutajwa tayari hayapingani na Amri za Mungu moja kwa moja. Hatuna amri yo yote kuhusu uadhimishaji wa ufufuo au kuzaliwa kwa Kristo. Tunaweza kutafakari juu ya ufufuo Wake na kuzaliwa Kwake kwa wakati wo wote ule na katika siku yo yote ile ya mwaka. Katika sura inayofuata tutagundua kwamba mafundisho mengine ya kipagani yaliingizwa [kanisani] ambayo yanaondoa moyo wa dini ile ya kweli ya Biblia. Hatuyashughulikii sana [mambo hayo], isipokuwa mambo yale tu yanayokiuka amri ya wazi ya Mungu.

Mamlaka ya Upapa iliyokuwa inakua iliendelea na programu yake ya kuweka mafundisho mengine ya uongo kinyume na kweli zile zilizomo katika Neno la Mungu. Macho yetu na yafumbuke ili tupate kuyatambua mafundisho hayo ya uongo na kuendelea kuwa watiifu kwa ile kweli halisi katika mfumo wake wa asili.

Related Information