JE, KRISTO NI MUNGU?
Mahali pengi katika Biblia Kristo anaitwa Mungu. Mtunga Zaburi anasema: "Mungu, Mungu BWANA (YEHOVA), amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake. Tokea Sayuni ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika. Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza, Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote. Ataziita mbingu zilizo juu, na nchi pia awahukumu watu wake. Nikusanyieni wacha Mungu wangu wanaofanya agano nami kwa dhabihu. Na mbingu zitatangaza haki yake, kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu." Zaburi 50: 1 - 6.
Kwamba fungu hili linamhusu Yesu huweza kufahamika (1) kwa ukweli ambao tayari tumejifunza, kwamba hukumu yote amempa Mwana; tena (2) ukweli kwamba ni wakati ule wa kuja kwake mara ya pili atakapowatuma malaika zake kuwakusanya wateule wake kutoka pepo nne za dunia. Mt.24:3l. "Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza." La; Bwana Mwenyewe atakaposhuka kutoka mbinguni, itakuwa "pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu." 1 The.4:16. Mwaliko huu utakuwa ni sauti ya Mwana wa Mungu, ambayo wote walio makaburini wataisikia, nayo itawafanya watoke. Yohana 5:28,29. Pamoja na wenye haki walio hai watanyakuliwa na kumlaki Bwana hewani, na hivyo kuwa pamoja na Bwana milele; na tukio hilo litafanya "kukusanyika kwetu mbele zake." 2 The.2:1. Linganisha Zab.50:5; Mt.24:31, na l The.4:16.
"Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote;" kwa maana Bwana Yesu atakapofunuliwa kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake, itakuwa "katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu." 2 The.1:8. Hivyo, basi, tunajua ya kuwa Zab.50:1-6 ni maelezo yaliyo dhahiri juu ya kuja kwake Kristo mara ya pili kwa wokovu wa watu Wake. Atakapokuja atakuwa kama "Mungu Mwenye nguvu." Linganisha na Habakuki 3.
Hiki ni kimojawapo cha vyeo vyake halali. Muda mrefu kabla ya kuja kwa Yesu mara ya kwanza, nabii Isaya alisema maneno haya ya faraja kwa Israeli: "Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani." Isa.9:6.
Haya siyo tu maneno yake Isaya; ni maneno ya Roho wa Mungu. Katika hotuba yake ya moja kwa moja aliyotoa kwa Mwanawe, Mungu amemwita kwa cheo kile kile kimoja. Katika Zab.45:6 tunasoma maneno haya: "Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili." Msomaji wa juu-juu tu angeweza kuyachukulia maneno hayo kuwa ni kumtolea tu sifa Mungu kulikofanywa na Mtunga Zaburi; lakini tunapoligeukia Agano Jipya, tunaona ya kuwa ni zaidi ya hizo. Tunaona kwamba Mungu Baba ndiye mnenaji, na kwamba anazungumza na Mwanawe, akimwita Mungu. Angalia Ebr.1:1-8.
Jina hili hakupewa Kristo kama matokeo ya mafanikio makubwa, bali ni lake kwa haki ya urithi. Akisema juu ya uweza na ukuu wake Kristo, mwandishi kwa Waebrania anasema kwamba amefanyika bora kuliko malaika, kwa sababu ya "jina ALILORITHI lilivyo tukufu kuliko lao." Ebr .1 :4. Mwana siku zote hutwaa jina la baba yake kihalali; naye Kristo, kama "Mwana pekee wa Mungu," analo jina lile lile kihalali. Pia mwana kwa sehemu kubwa au ndogo ni chapa ya baba yake; kwa kiwango fulani ana sura na tabia kama ya baba yake; si kwa ukamilifu, kwa vile hakuna kufanana kabisa miongoni mwa wanadamu. Lakini kwa Mungu hakuna hali ya kutokuwa na ukamilifu, au katika kazi zake zote; na kwa ajili hiyo Kristo ni "Chapa" ya nafsi ya Baba yake. Ebr.1:3. Yeye akiwa Mwana wa Mungu aliyeko milele, kwa asili anazo tabia zote za Mungu.
Ni kweli kwamba kuna wana wengi wa Mungu; bali Kristo ndiye "Mwana pekee wa Mungu," na kwa ajili hiyo ni Mwana wa Mungu kwa maana ile ambayo kiumbe kingine cho chote hakikupata au hakiwezi kuwa. Malaika ni wana wa Mungu, kama vile alivyokuwa Adamu (Ayubu 38:7; Luka 3:38) kwa uumbaji; Wakristo ni wana wa Mungu kwa kufanywa wana (Rum.8:l4,l5); lakini Kristo ni Mwana wa Mungu kwa kuzaliwa. Mwandishi kwa Waebrania anazidi kuonyesha kwamba cheo hiki cha Mwana wa Mungu sio kwa kupandishwa cheo Kristo, bali ni chake kwa haki. Anasema kwamba Musa alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, kama mtumishi, "bali Kristo, kama Mwana, juu ya nyumba ya Mungu." Ebr.3:6. Tena anasema pia kwamba Kristo ndiye Aitengenezaye nyumba. Fungu la 3. Yeye ndiye Alijengaye Hekalu la BWANA, na kuuchukua huo utukufu. Zek.6:12,13.
Kristo Mwenyewe alifundisha kwa kukazia sana kwamba Yeye ni Mungu.Yule kijana alipokuja kwake na kumwuliza, "Mwalimu mwema nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?" Yesu , kabla hajajibu swali lililokuja moja kwa moja kwake, alisema: "Kwa nini kuniita mwema? hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Marko 10:17,18. Hivi Yesu alikuwa na maana gani kusema maneno haya? Je, alikuwa na maana ya kukana jina hilo la sifa kuwa halimhusu Yeye? ----- La, hasha; kwa maana Kristo alikuwa mwema kabisa. Kwa Wayahudi wale, waliomwangalia sana daima kutaka kupata kasoro yo yote ndani yake ili wapate kumshtaki, aliwaambia kwa ujasiri, "Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Yohana 8:46. Katika taifa zima la Kiyahudi hapakuwa na mtu hata mmoja aliyepata kumwona akifanya jambo lo lote lenye mwelekeo wa dhambi; na wale waliokaza nia zao kumlaumu waliweza kufanya hivyo tu kwa kuwakodisha mashahidi wa uongo dhidi yake. Petro anasema kwamba Yeye "hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake." 1 Pet. 2:22. Paulo anasema kwamba "Yeye asiyejua dhambi." 2 Kor.5;21. Mtunga Zaburi anasema kwamba Yeye ni "Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu." Zab.92:l5. Naye Yohana anasema, "Nanyi mnajua ya kuwa Yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake." 1 Yohana 3:5.
Kristo hawezi kujikana Mwenyewe, kwa hiyo asingeweza kusema kwamba Yeye hakuwa mwema. Yeye ni na alikuwa mwema kabisa, ndiye utimilifu wa wema. Na kwa vile hakuna aliye mwema ila Mungu, na Kristo ni mwema, basi, inafuata kwamba Kristo ni Mungu, na ya kuwa hiyo ndiyo maana aliyotaka kumfundisha yule kijana.
Ilikuwa ni kwa maana iyo hiyo aliwafundisha wanafunzi wake. Filipoalipomwambia Yesu, "Utuonyeshe Baba, yatutosha," Yesu alimwambia: "Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyenion mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?" Yohana 14:8,9. Huu ni usemi wa mkazo sawa na ule aliosema, "Mimi na Baba tu umoja." Yohana 10:30. Kwa hiyo Kristo alikuwa Mungu kweli, hata wakati ule alipokuwa hapa miongoni mwa watu, alipoulizwa kuwaonyesha Baba aliweza kusema, Niangalie Mimi. Basi hilo linatukumbusha usemi usemao kwamba Baba alipomleta Mzaliwa wa Kwanza ulimwenguni, alisema, "Na wamsujudu malaika wote wa Mungu." Ebr.1:6. Haikuwa wakati ule tu Kristo aliposhiriki utukufu wa Baba kabla ya ulimwengu huu kuwako alipostahili kusujudiwa, bali hata alipokuja kama Mtoto Mchanga kule Bethlehemu, hata wakati huo malaika wote wa Mungu waliagizwa kumsujudu.
Wayahudi hawakukosa kuyaelewa mafundisho yake Kristo kumhusu Yeye Mwenyewe. Alipotangaza kwamba Yeye alikuwa umoja na Baba yake, Wayahudi waliokota mawe na kutaka kumpiga nayo; naye alipowauliza kwa kazi ipi njema walitafuta kumpiga kwa mawe, walijibu, "Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe, bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu." Yohana 10:33. Angekuwa kama vile walivyomdhania, yaani, mwanadamu tu, basi, maneno Yake kwa kweli yangekuwa kukufuru; walakini Yeye alikuwa Mungu.
Kusudi la Kristo kuja duniani lilikuwa ni kumfunua Mungu kwa wanadamu, ili kwamba wapate kuja kwake. Kwa hiyo mtume Paulo anasema kwamba "Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake (2 Kor.5:l9); na katika Yohana tunasoma kwamba yule Neno, aliyekuwa Mungu "alifanyika mwili." Yohana 1:1,14. Katika kuunganisha na wazo hilo yasemekana kwamba, "Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua" (au kumfanya ajulikane). Yohana 1:l8.
Angalia usemi huu, "Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba." Anayo makao yake pale, naye YUKO pale kama sehemu ya Uungu, kwa hakika alivyokuwa hapa duniani kama alivyo huko mbinguni. Matumizi ya usemi wake katika wakati wa sasa humaanisha kuendelea kuwako kwake. Unatoa wazo lile lile linalopatikana katika usemi wa Yesu kwa Wayahudi (Yohana 8:58), "Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko." Jambo hilo huonyesha tena kujilinganisha kwake na yule Mmoja aliyemtokea Musa katika kijiti kile kilichowaka moto, aliyelitangaza jina lake kuwa ni "MIMI NIKO AMBAYE NIKO."
Basi, hatimaye tunayo maneno yaliyovuviwa ya mtume Paulo yanayomhusu Yesu Kristo, kwamba "katika Yeye ilipendeza utimilifu wote ukae." Kol.1:19. Utimilifu huu ulivyo, unaokaa ndani yake Kristo, ni somo tunalojifunza katika sura inayofuata; ambamo tunaambiwa kwamba, "katika Yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili." Kol.2:9. Huu ni ushuhuda ulio kamili na wazi kabisa unaoonyesha ukweli kwamba Kristo kwa asili anazo tabia zote za Mungu. Ukweli huu kuhusu Uungu wake Kristo pia utazidi kuonekana kwa dhahiri sana kadiri tutakavyoendelea kumtafakari.