MAFUNDISHO MUHIMU YA KUTUMIA KATIKA MAISHA YETU
Hii siyo tu nadharia nzuri, au fundisho la kanuni tu, kwamba tungemtafakari Kristo kama Mungu na Muumbaji. Kila fundisho la Biblia tukilitumia ni kwa manufaa yetu, nalo lingejifunzwa kwa kusudi hilo. Hebu kwanza tuone fundisho hili lina uhusiano gani na amri ile ya katikati ya Sheria ya Mungu. Katika Mwanzo 2:1-3 tunayakuta maneno haya ya kufungia ukumbusho wa uumbaji: "Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya." Tafsiri ya Kiyahudi inaliweka fungu hili kwa kutumia tafsiri hii ya neno moja moja: "Basi zikamalizika mbingu na nchi, na jeshi lake lote. Naye Mungu alimaliza siku ya saba kazi yake aliyoifanya, n.k.. Hii ni sawa na ile tunayoipata katika amri ya nne, Kut.20:8-11.
Katika hiyo tunaliona jambo ambalo ni la kawaida kabisa, kwamba ni Yule yule Aliyeumba, ambaye alistarehe. Yule yule aliyefanya kazi kwa siku sita kuiumba nchi hii, ndiye aliyestarehe siku ya saba na kuibarikia na kuitakasa. Lakini tumekwisha jifunza tayari kwamba Mungu Baba aliuumba ulimwengu kwa njia ya Mwanawe Yesu Kristo, na ya kwamba Kristo aliumba kila kitu kilichopo. Kwa hiyo mwisho usioweza kuepukika ni kwamba Kristo ndiye aliyestarehe siku ile ya saba ya mwanzo, mwishoni mwa siku zile sita za uumbaji, na ya kwamba ndiye aliyeibarikia na kuitakasa. Hivyo siku ya saba --- Sabato ---- bila shaka lo lote ndiyo Siku ya Bwana. Yesu aliposema kwa Mafarisayo waliozozana naye maneno haya, "Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato"(Mt.12:8), alikuwa anatangaza Ubwana wake juu ya siku ile ile ambayo kwa desturi wao waliitunza kwa uangalifu sana; naye alifanya hivyo kwa maneno yanayoonyesha kwamba aliiheshimu kama alama ya mamlaka yake, ikithibitisha ukweli kwamba Yeye alikuwa mkuu kuliko Hekalu. Hivyo, siku ya saba imewekwa na Mungu kuwa ukumbusho wa uumbaji. Ni siku inayoheshimiwa kuliko siku zote, kwa vile kazi yake ya pekee ni kukumbusha juu ya uweza wa uumbaji wa Mungu, ambao ni mojawapo ya ushuhuda kwa mwanadamu juu ya Uungu wake. Basi, hapo Kristo aliposema kwamba Mwana wa Adamu ni BWANA WA SABATO, alikuwa anadai heshima ya juu ---- sio chini ya kuwa Muumbaji, ambaye Uungu wake siku hiyo inasimama kama ukumbusho wake.
Tutasemaje, basi, kwa shauri ambalo huwa linatolewa mara kwa mara, kwamba Kristo alibadili Siku ya Sabato kutoka siku ile inayofanya ukumbusho wa uumbaji kamili kwenda siku isiyokuwa na maana kama hiyo? Jibu ni rahisi, kama Kristo angeweza kubadili au kutangua Sabato, basi, angekuwa ameiharibu kazi ya mikono Yake Mwenyewe, angekuwa amefanya kazi kinyume chake Mwenyewe; na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hautasimama. Walakini, Kristo "hawezi kujikana Mwenyewe," na kwa ajili hiyo Yeye Mwenyewe alikiamuru, kile ambacho, kwa ajili ya kushuhudia Uungu Wake, humdhihirisha Yeye kuwa anastahili heshima kuliko miungu yote ya kishenzi. Lingekuwa jambo lisilowezekana kabisa kwa Kristo kubadili Sabato kama vile ingalivyokuwa kubadili ukweli kwamba aliviumba vitu vyote kwa siku sita, na kustarehe siku ya saba.
Tena maneno yale yanayorudiwa mara kwa mara kwamba Bwana ni Muumbaji yamekusudiwa kuwa chimbuko la nguvu. Angalia jinsi uumbaji na ukombozi vilivyounganishwa pamoja katika sura ya kwanza ya Wakolosai. Kupata wazo kamili lililo mbele yetu tutasoma mafungu kuanzia la 9 mpaka l9:-
"Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu Wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika Yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia Yake, na kwa ajili Yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika Yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha Kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika Yeye ilipendeza utimilifu wote ukae."
Sio bahati mbaya kwamba maneno ya ajabu yanayomhusu Kristo kama Muumbaji yameunganishwa na usemi kwamba katika Yeye tuna ukombozi. Si hivyo tu; mtume anapotujulisha tamaa yake kwamba sisi tunge "Wezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu Wake," anatujulisha nguvu ile ni nini. Anapotuambia juu ya kuokolewa katika nguvu za giza, anatufahamisha jambo fulani kuhusu uweza wa Mkombozi huyo. Ni kwa faraja yetu kwamba tunaambiwa kwamba kichwa cha kanisa ni Muumbaji wa vitu vyote. Tunaambiwa kwamba Yeye anavichukua vitu vyote kwa amri ya uweza wake (Ebr.1:3), ili tupate kutulia katika ahadi isemayo kwamba
"Mkono ule unaovichukua viumbe vyote Utawalinda watoto wake vizuri."
Angalia uhusiano uliopo katika Isa.40:26. Sura hiyo inaeleza hekima ya ajabu na uweza Wake Kristo, kwa kuweza kuliita jeshi lote la mbinguni kwa majina, na kwa kulishikilia mahali pake, kwa ukuu wa uweza wake na nguvu ya uweza Wake, kisha anauliza swali: "Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie? Je! wewe hukujua? hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki." Na kinyume chake Yeye "Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo." Uweza wake, kwa kweli, ni uwezo wake wa kuumba kila kitu pasipo kutumia kitu kingine cho chote; kwa hiyo anaweza kufanya maajabu ndani ya wale wasiokuwa na nguvu. Anaweza kuongeza nguvu pale pasipokuwa na nguvu. Basi, ni hakika kitu cho chote kinachosaidia kuweka mioyoni mwetu ukumbusho wa uweza wake Kristo wa uumbaji, sharti kiifanye upya nguvu yetu ya kiroho pamoja na kutupatia ujasiri.
Na hili ndilo kusudi la Sabato. Soma Zaburi 92 ambayo imepewa kichwa cha Zaburi kwa ajili ya Siku ya Sabato. Mafungu manne ya mwanzo ni haya:
"Ni neno jema kumshukuru Bwana, na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu. Kuzitangaza rehema zako asubuhi, Na uaminifu wako wakati wa usiku. Kwa chombo chenye nyuzi kumi, Na kwa kinanda, Na kwa mlio wa kinubi. Kwa kuwa umenifurahisha, Bwana, Kwa kazi yako; nitashangilia Kwa ajili ya matendo ya mikono yako."
Maneno haya yana uhusiano gani na Sabato? Jibu ni hili: Sabato ni ukumbusho wa uumbaji. Asema Bwana: "Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye." Eze.20:12. Mtunga Zaburi huyu aliitunza Sabato kama vile Mungu alivyokusudia kuwa itunzwe ---- kwa kutafakari juu ya uumbaji na uweza wake wa ajabu na fadhili zake Mungu zinazodhihirishwa kwa huo. Halafu, kwa kutafakari hayo, alitambua kwamba Mungu anayeyavika hivi maua ya mashambani kwa uzuri unaozidi ule wa Sulemani, anavijali zaidi sana viumbe vyake vyenye akili; naye alipoziangalia mbingu, zinazoonyesha uweza na utukufu wa Mungu, alitambua kwamba ziliumbwa kutoka pasipo kitu, wazo hili lenye kutia matumaini lingemjia na kumkumbusha kuwa uweza ule ule ungeweza kufanya kazi ndani yake na kumkomboa kutokana na udhaifu wa kibinadamu aliokuwa nao. Kwa hiyo, alifurahi, na kushangilia kwa ajili ya matendo ya mikono Yake Mungu. Maarifa na Uweza wa Mungu vilivyomjia kwa njia ya kutafakari uumbaji, vikamjaza matumaini alipotambua kwamba uweza ule ule ulikuwa mkononi mwake; naye, akiwa ameushika uweza ule kwa imani, alipata ushindi kwa njia Yake. Na hili ndilo kusudi la Sabato; inamleta mtu kuyapata maarifa yale yaokoayo ya Mungu.
Kwa maelezo mafupi, hoja hasa ni hii: 1. Imani kwa Mungu hutokana na ujuzi wa Uweza Wake; kutomwamini Yeye huonyesha ujinga wa kutokujua uweza wake wa kuweza kuzitimiza ahadi Zake; imani yetu kwake haina budi kuwa katika kiwango kile kile cha ujuzi wetu halisi wa Uweza Wake. 2. Kuutafakari uumbaji wa Mungu kwa akili zetu hutupatia dhana ya kweli ya uweza Wake; kwa vile uweza wake wa milele na Uungu wake hueleweka kwetu kwa njia ya vitu alivyoviumba. Rum.1:20. 3. Ni imani inayotupatia ushindi (1 Yohana 5:4); basi, kwa kuwa imani huja kwa kujifunza uweza wa Mungu, kutokana na Neno lake na vitu vile alivyoviumba, tunapata ushindi au tunashangilia kwa njia ya matendo ya mikono Yake. Basi, Sabato, ambayo ni ukumbusho wa uumbaji, ikitunzwa vizuri, ni chimbuko kuu kuliko yote la kumtia Mkristo nguvu mpya katika mapambano yake.
Hii ndiyo maana ya Eze. 20:12: "Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye." Yaani, kujua kuwa utakaso wetu ndiyo mapenzi yake Mungu (1 The.4:3; 5:23,24), sisi, kwa njia ya Sabato kama ikitunzwa vizuri, tunajifunza jinsi uweza wa Mungu unaotumika kwa utakaso wetu ulivyo. Uweza ule ule uliotumika kuumba ulimwengu umetolewa sasa kwa ajili ya utakaso wa wale wanaojitoa nafsi zao wenyewe kufanya mapenzi ya Mungu. Kwa kweli wazo hili, likizingatiwa kikamilifu, bila shaka litaweza kuleta furaha na faraja katika Mungu kwa roho ile inayoipenda kweli. Kwa nuru hii, tunaweza kutambua nguvu iliyomo katika Isa. 58:l3,l4:-
"Kama ukigeuza mguu wako usiihalifu Sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita Sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima, ukiitukuza, kwa kutozifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; NDIPO UTAKAPOJIFURAHISHA KATIKA BWANA; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo."
Yaani, Sabato ikitunzwa kulingana na mpango wa Mungu, kama ukumbusho wa Uweza Wake wa uumbaji, ikitukumbusha pia juu ya uweza wa Mungu unaotolewa kwa ajili ya wokovu wa watu wake, basi, roho ile, itakayoshangilia matendo ya mikono Yake, haitakosa kujifurahisha yenyewe katika Bwana. Hivyo, Sabato ni egemeo kuu la wenzo ya imani, inayoiinua juu roho ile kukifikia kimo cha kiti cha enzi cha Mungu, na kuzungumza naye.
Kuliweka suala hili kwa maneno machache, yaweza kusemwa hivi: Uweza wa milele na Uungu wa Bwana hudhihirika katika uumbaji. Rum.1:20. Ni uwezo ule ule wa kuumba ambao unapima uweza wa Mungu. Lakini Injili ni uweza wa Mungu uuletao wokovu. Rum.l:l6. Kwa hiyo, Injili inatuonyesha sisi uwezo ule tu uliotumika katika kuumba ulimwengu, ambao sasa unatumika kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Ni uweza ule ule kwa kila hali.
Katika nuru ya ukweli huu mkuu, hakuna nafasi ya majadiliano juu ya kama ukombozi ni mkuu kuliko uumbaji, kwa sababu ukombozi NI uumbaji. Angalia 2 Kor.5:l7; Efe.4:24. Uweza wa ukombozi ni uweza ule ule wa uumbaji; uweza wa Mungu uuletao wokovu ni uweza ule ule unaoweza kuufanya ubinadamu ambao si kitu kuwa kitu kile ambacho kitakuwa sifa ya utukufu wa neema yake Mungu milele hata milele. "Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba Mwaminifu." 1 Pet.4:l9.