KRISTO MTOA SHERIA
"Kwa maana BWANA ndiye mwamuzi wetu; BWANA ndiye Mfanya [Mtoa] sheria wetu; BWANA ndiye Mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa." Isa.33:22.
Sasa tunapaswa kumtafakari Kristo katika tabia yake nyingine, walakini sio tabia nyingine. Ni moja ambayo inatokana na cheo chake cha Muumbaji, kwa vile yule Mmoja anayeumba sharti awe na mamlaka ya kuongoza na kutawala. Tunasoma maneno yake Kristo katika Yohana 5:22,23 kwamba, "Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka." Kristo alivyo ufunuo wa Baba katika uumbaji, ndivyo alivyo ufunuo wa Baba katika kuitoa na kuitimiliza sheria. Mafungu haya machache ya Maandiko yatatosha kuwa uthibitisho.
Katika Hesabu 21:4-6 tunayo taarifa kwa sehemu tu ya tukio lililotokea wakati wana wa Israeli walipokuwa jangwani. Hebu na tuisome: "Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka katika nchi ya Misri, ili tufe jangwani? maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa." Watu wakamnung'unikia Mungu na Musa, wakisema; Mbona mmetupandisha huku jangwani? Wakamlaumu Kiongozi wao. Hii ndiyo sababu waliharibiwa na zile nyoka. Sasa soma maneno ya mtume Paulo kuhusu tukio hili:-
"Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka." 1 Kor.10:9. Maneno haya yanathibitisha nini? ---- Kwamba Kiongozi waliyekuwa wanamnung'unikia alikuwa ni Kristo. Maneno hayo yanathibitisha zaidi ukweli kwamba Musa alipochagua kuwa pamoja na Israeli, akikataa kuitwa mwana wa binti Farao, alihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri. Ebr.ll:26. Soma pia 1 Kor.10:4, Paulo asemapo ya kuwa baba zetu "Wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea Mwamba wa roho uliowafuata; na Mwamba ule ulikuwa ni Kristo." Hivyo, basi, Kristo alikuwa ndiye Kiongozi wa Israeli kutoka Misri.
Sura ya tatu ya Waebrania inauweka wazi ukweli uo huo. Hapa tunaambiwa kumtafakari Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu [Kristo], aliyekuwa Mwaminifu katika nyumba Yake yote, si kama mtumishi, bali kama Mwana, juu ya nyumba Yake Mwenyewe. Fungu la l-6. Kisha tunaambiwa ya kwamba sisi ni nyumba Yake kama tukishikamana sana na ujasiri wetu mpaka mwisho. Kwa hiyo tunaonywa na Roho Mtakatifu kuisikia sauti Yake na kutoifanya mioyo yetu migumu, kama baba zetu walivyofanya jangwani. "Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho; hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti Yake [Kristo], Msifanye migumu mioyo yenu, kama wakati wa kukasirisha. Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa? Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?" Fungu la 14-17. Hapa tena Kristo anaonekana kuwa Yeye ndiye Kiongozi na Amiri Jeshi (Kamanda) wa Israeli katika miaka yao arobaini ya kukaa jangwani.
Jambo lilo hilo linaonekana katika Yoshua 5:13-15, ambapo tunaambiwa ya kwamba mtu yule aliyemwona Yoshua karibu na Yeriko, akiwa na upanga wazi mkononi mwake, akijibu swali hili la Yoshua alilomwuliza, "Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu!" akasema, "La, lakini nimekuja sasa, nili Amiri wa Jeshi la BWANA." Naam, hapatakuwa na mtu ye yote anayebisha kwamba Kristo alikuwa Kiongozi halisi wa Israeli, japokuwa alikuwa haonekani kwa macho. Ni Kristo aliyemwamuru Musa kwenda kuwaokoa watu Wake. Sasa soma Kutoka 20:1-3:-
"Mungu akanena maneno haya yote akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila Mimi." Je, ni nani aliyanena maneno haya? ---- Ni Yule aliyewatoa katika nchi ya Misri. Tena ni nani aliyekuwa Kiongozi wa Israeli kutoka Misri? --- Alikuwa ni Kristo. Ni nani, basi, aliyenena sheria kutoka katika Mlima ule wa Sinai? ---- Alikuwa ni Kristo, mng'ao wa utukufu wa Baba, na Chapa ya nafsi Yake, ambaye ndiye ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu. Alikuwa ni yule Muumbaji wa viumbe vyote vilivyoumbwa, na ndiye yule yule aliyepewa hukumu yote.
Hoja hii yaweza kuthibitishwa kwa njia nyingine. Hapo Bwana ajapo, itakuwa kwa mwaliko (l The.4:l6), ambao utapenya makaburi na kuwaamsha wafu (Yohana 5:28,29). "BWANA atanguruma toka juu, Naye atatoa sauti yake toka patakatifu pake; Atanguruma sana juu ya zizi lake; Atapiga kelele kama mtu akanyagaye zabibu, Juu ya wenyeji wote wa dunia. Mshindo utafika hata mwisho wa dunia; Maana BWANA ana mashindano na mataifa, Atateta na watu wote wenye mwili; Na waovu atawatoa wauawe kwa upanga; asema BWANA." Yer.25:30,3l. Tukilinganisha maneno hayo na yale ya Ufunuo l9:ll-2l, tunamwona Kristo akiwa Kiongozi wa majeshi yaliyo mbinguni, Neno la Mungu, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana, anatoka kulikanyaga hilo shinikizo kubwa la zabibu la ghadhabu ya Mungu, akiwaangamiza waovu wote, tunagundua kwamba ni Kristo anayenguruma toka katika patakatifu pake juu ya wenyeji wote wa dunia, atakapokuwa na mashindano na mataifa yote. Yoeli anaongeza wazo jingine anaposema, "Naye BWANA atanguruma toka Sayuni, atatoa sauti yake toka Yerusalemu; na mbingu na nchi zitatetemeka." Yoeli 3:l6.
Kutokana na mafungu haya, ambayo yanaweza kuongezewa mengine juu yake, tunajifunza ya kwamba, kuhusiana na marejeo ya Bwana kuja kuwakomboa watu Wake, atanena kwa sauti inayoitetemesha nchi na mbingu, ---- "Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawayawaya kama machela [nayo itaondolewa kama kibanda]" (Isa.24:20), nazo "Mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu" (2 Petro 3:l0). Hebu sasa soma Waebrania l2:25,26:-
"Angalieni msimkatae Yeye anenaye. Maana ikiwa hawakuokoka wale waliomkataa Yeye aliyewaonya juu ya nchi, zaidi sana hatutaokoka sisi tukijiepusha na Yeye atuonyaye kutoka mbinguni; ambaye sauti Yake iliitetemesha nchi wakati ule; lakini sasa ameahidi akisema, Mara moja tena nitatetemesha si nchi tu, bali na mbingu pia."
Wakati Sauti hii iliponena juu ya nchi na kuitetemesha nchi ulikuwa ni wakati ule wa kuinena Sheria toka Sinai (Kut.l9:l8-20; Ebr.l2:l8-20), tukio ambalo kutisha kwake halina kifani, wala halitakuwa nacho mpaka hapo Bwana atakapokuja na malaika wote wa mbinguni kuwaokoa watu Wake. Lakini zingatia maneno haya: Sauti ile ile iliyoitetemesha nchi wakati ule itatetemesha si nchi tu, bali na mbingu pia wakati huo ujao; nasi tumekwisha kuona ya kwamba ni Sauti Yake Kristo itakayosikika kwa kelele kubwa kiasi cha kuitetemesha mbingu na nchi hapo atakapokuwa na mashindano na mataifa. Basi, imethibitishwa kwamba ilikuwa ni Sauti Yake Kristo iliyosikika pale Sinai, ikitangaza Amri Kumi. Hitimisho la hoja hii si zaidi ya vile ambavyo kwa kawaida lingeweza kufikiwa kutokana na yale tuliyokwisha kujifunza juu yake Kristo kama Muumbaji, na Mwanzilishi wa Sabato.
Naam, ukweli usemao kwamba Kristo ni sehemu ya Uungu, Mwenye sifa zote za Mungu, Aliye sawa na Baba kwa hali zote, Muumbaji na Mtoa Sheria, ndiyo nguvu pekee iliyomo ndani ya upatanisho. Hiyo ndiyo peke yake inafanya ukombozi uwezekane. Kristo alikufa "ili atulete kwa Mungu" (l Petro 3:l8); walakini kama angepungua hata kwa nukta moja tu katika usawa wake na Mungu, asingeweza kutuleta sisi Kwake. Uungu maana yake ni kuwa na tabia za Mungu. Kama Kristo asingekuwa Mungu, basi, tungekuwa tumepata kafara ya kibinadamu tu. Si kitu, hata kama tukikubali kwamba Kristo alikuwa kiumbe cha juu sana chenye akili kilichoumbwa katika ulimwengu, katika hali hiyo angekuwa mtu tu, mwenye kuwiwa utii kwa Sheria, asingekuwa na uwezo wa kufanya zaidi ya wajibu wake. Asingekuwa na haki ya kuwagawia watu wengine. Kuna umbali usiopimika kati ya malaika wa cheo cha juu sana aliyepata kuumbwa, na Mungu; hivyo hata malaika wa cheo cha juu mno asingeweza kumwinua juu mwanadamu aliyeanguka dhambini, na kumfanya apate kushiriki tabia ya Uungu. Malaika wanaweza tu kuhudumu; Mungu peke yake anaweza kukomboa. Mungu na ashukuriwe kwa kuwa tunaokolewa "kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu," ambaye katika Yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili; na, kwa ajili hiyo, awezaye kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa Yeye.
Ukweli huu hutusaidia kupata ufahamu kamili wa sababu kwa nini Kristo huitwa Neno la Mungu. Yeye ndiye kupitia Kwake mapenzi ya Mungu na Uweza wa Mungu hujulikana kwa wanadamu. Tuseme hivi, Yeye ndiye kinywa cha Mungu, Ufunuo wa Mungu. Anamtangaza ama anamfunua Mungu kwa mwanadamu. Ilimpendeza Baba kwamba ndani Yake utimilifu wote ukae; na kutokana na sababu hiyo, Baba hajawekwa katika cheo kilicho duni, kama wengine wanavyodhani, Kristo anapotukuzwa kama Muumbaji na Mtoa Sheria; kwa maana utukufu wa Baba unang'aa kupitia kwa Mwanawe. Kwa kuwa Mungu anajulikana tu kwa njia yake Kristo, basi, ni dhahiri ya kwamba Baba hawezi kuheshimiwa kama anavyostahili kuheshimiwa na wale ambao hawamtukuzi Kristo. Kama vile Kristo Mwenyewe alivyosema, "Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka." Yohana 5:23.
Je, hivi swali linaulizwa kwamba Kristo angewezaje kuwa Mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu na pia kuwa Mtoa Sheria? Haitupasi sisi kueleza jinsi jambo hilo linavyoweza kuwa, bali inatupasa kuikubali kumbukumbu ya Maandiko tu kuwa ndivyo ilivyo. Na ukweli huu kwamba ndivyo ilivyo ndio unaolipa nguvu fundisho hili la upatanisho. Dhamana ya mwenye dhambi ya msamaha kamili, utolewao bure, hukaa katika ukweli huu kwamba Mtoa Sheria Mwenyewe, Yule ambaye amemwasi na kutaka kupigana naye, huyo ndiye Yule yule aliyejitoa Mwenyewe kwa ajili yetu. Yawezekanaje, basi, kwa ye yote kutilia mashaka unyofu wa kusudi lake Mungu, wakati Yeye alijitoa Mwenyewe kwa ajili ya ukombozi wao? maana isifikiriwe ya kwamba Baba na Mwana walitengana katika jambo hili. Walikuwa umoja katika jambo hili, kama ilivyo kwa kila kitu kinginecho. Shauri la amani lilikuwa kati ya hao wawili (Zek.6:l2,l3), na hata Mwana Pekee alipokuwa hapa duniani alikuwa katika kifua cha Baba.
Ni ufunuo wa upendo wa ajabu ulioje! Yeye asiyekuwa na hatia aliteseka kwa ajili ya wenye hatia; Yeye Mwenye Haki, kwa ajili ya wale wasiokuwa na haki; Muumbaji, kwa ajili ya kiumbe; Mfanya [Mtoa] Sheria, kwa ajili ya yule anayeivunja sheria hiyo; Mfalme, kwa ajili ya raia zake waasi. Kwa kuwa Mungu hakumwachilia Mwana Wake Mwenyewe, bali alimtoa kwa hiari kwa ajili yetu sisi sote; ---- kwa kuwa Kristo alijitoa kwa hiari kwa ajili yetu sisi; ---- atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja Naye? Upendo usiokuwa na kikomo haukuweza kupata njia kuu zaidi ya ile ya kujifunua wenyewe kwetu sisi. Ni vyema kwamba Bwana aseme, "Je! ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda?"