MUNGU ADHIHIRISHWA KATIKA MWILI
"Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu. Yohana 1:l4.
Hakuna maneno mengine ambayo yangeweza kuonyesha kwa wazi zaidi kwamba Kristo alikuwa Mungu na mwanadamu kwa wakati mmoja. Kwa asili yake alikuwa ni Mungu tu, alitwaa asili ya kibinadamu na kutembea miongoni mwa wanadamu kama mwanadamu wa kawaida tu mwenye hali ya kufa, isipokuwa ni wakati ule tu Uungu wake ulipojitokeza, kama wakati ule wa tukio la kulitakasa hekalu, ama wakati ule maneno yake yenye kuchoma juu ya ukweli wake rahisi yalivyowafanya hata adui zake kukiri kwamba "Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena."
Kujinyenyekeza kwa hiari yake ambako Kristo alikuwa nako kumeelezwa vizuri sana na Paulo kwa Wafilipi: "Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye Yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya msalaba." Wafilipi 2:5-8, soma pambizo (katika 'Revised Version').
Tafsiri hiyo juu hulifanya fungu hili liwe wazi zaidi kuliko lilivyo katika tafsiri ya kawaida. Wazo lenyewe ni kwamba, ijapokuwa Kristo alikuwa yuna namna ya Mungu, akiwa "mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake" (Ebr.1:3), akiwa na sifa zote za Mungu, akiwa ndiye Mtawala wa ulimwengu na Mmoja ambaye wote Mbinguni humheshimu, hakuona kuwa jambo lo lote katika hayo lilikuwa la kutamanika kwake, kwa kadiri alivyowaona wanadamu walivyokuwa wamepotea na hawana nguvu.Asingeweza kufurahia utukufu wake wakati mwanadamu ametupwa nje, pasipo tumaini. Kwa hiyo, Alijifanya Mwenyewe kuwa si kitu, Alijivua Mwenyewe utajiri Wake wote pamoja na utukufu wake, akatwaa mfano wa mwanadamu, ili apate kumkomboa. Basi, katika hali hiyo, tunaweza kusuluhisha umoja uliopo kati ya Kristo na Baba kwa usemi huu, "Baba yangu ni mkuu kuliko Mimi."
Haiwezekani kwetu sisi kuelewa kwa jinsi gani Kristo, kama Mungu, angeweza kujinyenyekeza na kuwa mtii hata mauti ya msalaba, na kwetu sisi ni bure kabisa kujaribu kukisia jambo hilo lilivyo. Yote tunayoweza kufanya ni kuukubali ukweli kama ulivyotolewa katika Biblia. Kama msomaji anapata shida katika kuulinganisha baadhi ya usemi huu katika Biblia kuhusu asili yake Kristo, basi, hebu na akumbuke ya kwamba lingekuwa jambo lisilowezekana kuielezea kwa maneno ambayo wanadamu wenye akili finyu wangeweza kuzingatia kikamilifu. Kama vile ilivyo kinyume na maumbile kuwapandikiza watu wa Mataifa katika shina la Israeli, ndivyo mambo mengi katika nyumba ya Mungu yalivyo kitendawili kwa ufahamu wa kibinadamu.
Maandiko mengine tutakayodondoa yanaleta karibu zaidi nasi ukweli wa ubinadamu wake Kristo, na maana yake kwetu. Tumekwishasoma tayari kwamba "Naye Neno alifanyika mwili," na sasa hivi tutasoma yale asemayo Paulo kuhusu asili ya mwili ule: "Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe Mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili, ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho." Rum.8:3,4.
Wazo dogo tu litatosha kumwonyesha mtu ye yote kwamba kama Kristo alichukua mfano wa mwanadamu, ili apate kumkomboa mwanadamu huyo, basi, ni lazima alikuwa mwanadamu mwenye dhambi ambaye Yeye (Kristo) alitwaa mfano wake, kwa maana ni mwanadamu mwenye dhambi ambaye alikuja kumkomboa. Mauti isingekuwa na nguvu juu ya mtu asiyekuwa na dhambi, kama vile Adamu alivyokuwa katika Edeni; nayo isingeweza kuwa na nguvu yo yote juu yake Kristo, kama Bwana asingaliweka juu yake maovu yetu sisi sote. Zaidi ya hayo, ukweli kwamba Kristo alichukua juu yake mwili, sio ule wa kiumbe kisichokuwa na dhambi, bali wa mwanadamu mwenye dhambi, yaani, ya kwamba mwili ule aliouchukua ulikuwa na udhaifu wote na mwelekeo wa kutenda dhambi ambao anao kiasili mwanadamu aliyeanguka dhambini, hudhihirishwa kwa usemi ule usemao kwamba Yeye "Aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi KWA JINSI YA MWIL." Daudi alikuwa na tamaa zote za kibinadamu. Yeye mwenyewe anajisema hivi: "Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani." Zab.51:5.
Usemi ufuatao kutoka katika kitabu cha Waebrania uko wazi sana juu ya hoja hii:-
"Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa." Ebr.2:16-18.
Kama alifananishwa na ndugu zake katika mambo yote, basi, hapana budi aliteseka na udhaifu wote, naye alikabiliwa na majaribu yote ya ndugu zake. Mafungu mawili zaidi yanayolikazia jambo hili yatakuwa ushahidi wa kutosha juu ya hoja hii. Kwanza tunanukuu 2 Kor.5:21:-
"Yeye [Mungu] asiyejua dhambi alimfanya [Kristo] kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye."
Usemi huu una nguvu zaidi kuliko ule usemao kwamba alifanyika "katika mfano wa mwili wa dhambi." Alifanywa KUWA DHAMBI. Hapa kuna siri iliyo sawa na ile isemayo kwamba Mwana wa Mungu angekufa. Mwana Kondoo wa Mungu asiye na waa lo lote, asiyejua dhambi, alifanywa kuwa dhambi. Akiwa hana dhambi yo yote, hata hivyo alihesabiwa sio tu kwamba ni mwenye dhambi, bali alitwaa mwili wa dhambi hasa. YEYE alifanywa kuwa dhambi ili SISI tupate kuwa haki. Hivyo Paulo anasema kwa Wagalatia kwamba "Mungu alimtuma Mwanawe, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili tupate kupokea hali ya kuwa wana. Gal.4:4,5.
"Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa." "Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. Ebr.2:18; 4:15,16.
Neno moja zaidi, kisha tunaweza kujifunza fundisho zima kutokana na ukweli kwamba "Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu." Ilikuwaje, basi, kwamba Kristo aliweza kuwa "katika hali ya udhaifu" (Ebr.5:2), lakini hakujua dhambi? Wengine, baada ya kusoma mpaka hapa, huenda wamefikiri kwamba tulikuwa tunaikashifu tabia ya Yesu, kwa kumshusha chini kufikia hali ya chini ya mwanadamu mwenye dhambi. Kinyume chake, tunautukuza tu ule "uweza wa Mungu" aliokuwa nao Mwokozi wetu wa neema, ambaye Yeye Mwenyewe kwa hiari yake alijinyenyekeza na kufanana na mwanadamu mwenye dhambi, ili amtukuze mwanadamu kufikia kiwango cha utakatifu wake Mwenyewe usiokuwa na waa, ambao alikuwa nao licha ya hali ngumu sana alizokabiliana nazo. Ubinadamu wake uliuficha Uungu wake, ambao kwa huo aliunganishwa kabisa na Mungu asiyeonekana, na ambao ulikuwa na uwezo mwingi zaidi kupingana na udhaifu wa mwili. Katika maisha yake yote alikuwa na mapambano. Mwili, ukichochewa na adui wa haki yote, ulikuwa na mwelekeo wa kuanguka dhambini, lakini Uungu Wake haukuikaribisha tamaa yo yote mbaya hata kwa dakika moja, wala Uweza wake wa Uungu haukuyumba hata kwa dakika moja. Akiisha kuteseka hivyo katika mwili mateso yote yale wanayoweza kuteseka wanadamu wote, alirudi kwenye kiti cha enzi cha Baba akiwa hana waa lo lote kama vile alivyokuwa kabla ya kuyaacha makao ya kifalme huko juu kwenye utukufu. Alipolala kaburini, akiwa chini ya mamlaka ya mauti, "ilikuwa haiwezekani kushikiliwa huko nayo," kwa sababu Yeye "hakujua dhambi."
Lakini yawezekana mmoja atasema, "Kwangu mimi sioni faraja yo yote kwa maneno haya. Bila shaka, ninacho kielelezo, lakini siwezi kukifuata, kwa kuwa sina nguvu kama ile aliyokuwa nayo Kristo. Yeye alikuwa Mungu hata wakati ule alipokuwa humu duniani; mimi ni mwanadamu tu." Ndio, lakini unaweza kuwa na uwezo ule ule aliokuwa nao ukitaka. Yeye alikuwa "katika hali ya udhaifu," lakini Yeye "hakufanya dhambi," kwa sababu ya uweza wa Mungu uliokaa daima ndani yake. Sasa, basi, hebu sikiliza maneno yaliyovuviwa ya mtume Paulo, kisha ujifunze haki tunayopaswa kuwa nayo:-
"Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, MPATE KUTIMILIKA KWA UTIMILIFU WOTE WA MUNGU." Efe.3:14-19.
Ni nani ambaye angeweza kuomba zaidi ya hayo? Kristo, ambaye ndani yake unakaa utimilifu wote wa Mungu kwa jinsi ya kimwili, anaweza kukaa ndani ya mioyo yetu, ili tupate kujazwa na utimilifu wote wa Mungu. Ni ahadi ya ajabu jinsi gani! Yeye "anachukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu." Yaani, akiisha kuteseka yote yale ambayo mwili wa dhambi umerithi, anaelewa mambo yote, naye anajifananisha sana na watoto wake kiasi kwamba lo lote linalowasonga linafanya msongo uo huo juu yake, naye anajua kiasi gani cha nguvu ya Mungu kinahitajika kuupinga msongo huo; nasi kama kwa dhati tunataka kukataa "ubaya na tamaa za kidunia," Yeye anaweza na tena anatamani kutupa nguvu "kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo." Uweza wote ambao Kristo alikuwa nao ndani yake kwa silika yake, sisi tunaweza kuwa nao ukikaa ndani yetu kwa neema yake, kwa maana anatugawia bure juu yetu.
Basi, hebu na wajipe moyo hao waliochoka, walio dhaifu, na wale waliosetwa na dhambi. Hebu na wa"kikaribie kiti cha neema kwa ujasiri," ambako wanayo hakika ya kupewa neema ya kuwasaidia wakati wa mahitaji, kwa sababu hitaji hilo ndilo linalomgusa Mwokozi kwa wakati ule ule wa mahitaji. Yeye "anachukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu." Kama ingekuwa ni kweli kwamba aliteseka tu miaka elfu moja na mia nane iliyopita [1888], basi, tungekuwa na hofu kwamba huenda alikuwa amesahau udhaifu mwingineo; lakini sivyo ilivyo, jaribu lilo hilo likusongalo wewe linamgusa Yeye. Majeraha yake bado yangali mapya, naye yu hai siku zote ili awaombee.
Ni uwezekano mwingi wa ajabu ulioje unaomngoja Mkristo! Ni upeo wa utakatifu ulioje anaoweza kuufikia! Haidhuru kwa kiasi gani Shetani anaweza kupigana naye, akimshambulia mahali pale pale ambapo mwili wake ni dhaifu sana, anaweza kukaa chini ya uvuli wake Mwenyezi, na kujazwa na utimilifu wa nguvu zake Mungu. Mmoja aliye na nguvu kuliko Shetani anaweza kukaa ndani ya moyo wake daima; na kwa ajili hiyo, akiyaangalia mashambulio ya Shetani kana kwamba yumo mwenye ngome imara, anaweza kusema, "Nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu."